MADEREVA WA BAJAJI IRINGA WAELEZA FAIDA ZA KAZI YAO KATIKA MAENDELEO YA JAMII
Na Ester Sebastian (UOI) – Matukio Daima Media
Madereva wa bajaji katika kituo cha Miomboni, Mkoa wa Iringa, wameeleza kuwa kazi ya uendeshaji wa bajaji imekuwa msaada mkubwa katika kuboresha maisha yao, kuwaepusha na makundi hatarishi katika jamii pamoja na kuchangia maendeleo ya uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.
Akizungumza na Matukio Daima Media , dereva wa bajaji kutoka Kata ya Kihesa, Frendinand Machocheo, amesema kazi hiyo imemuwezesha kupata kipato cha uhakika kinachomsaidia kutimiza mahitaji ya kila siku na kuendesha familia yake.
Amesema kuwa kupitia kazi ya bajaji ameweza kulipa kodi, kuwalisha watoto wake na kuepuka kujiingiza katika vitendo viovu kama ujambazi na utapeli ambavyo mara nyingi huwafanya vijana kupoteza mwelekeo wa maisha.
“Kazi ya bajaji imenifanya niheshimike nyumbani na katika jamii. Kijana asiye na kazi mjini huonekana hana mwelekeo wala thamani, lakini bajaji imenipa nafasi ya kujitegemea,” amesema Machocheo.
Kwa upande wake, dereva wa bajaji wa Miomboni, Ombeni Mahund, amesema kazi hiyo inamuwezesha kukidhi mahitaji muhimu ya binadamu ikiwemo chakula, mavazi na makazi.
“Kazi yangu ya bajaji inanisaidia kupata hela ya kula, kuvaa, kulipa ushuru wa barabarani na kuendesha maisha kwa ujumla,” amesema Mahund.
Naye dereva wa bajaji kutoka Tumaini, Elly Ng’umbi, amesema kazi hiyo imemsaidia kuepuka matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vya wizi, huku ikimpa muda mdogo wa kujihusisha na mambo yasiyo na tija kwa jamii.
“Mimi kama kijana, kazi ya bajaji imenisaidia kupata hela ya kupanga, kula, kuvaa na kugharamia mahitaji mengine ya kijamii. Pia inanifanya niwe bize muda wote na kuniepusha na vitendo visivyofaa katika jamii,” amesema Ng’umbi.
Madereva hao wametoa wito kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha vijana kupata stahiki zao na fursa mbalimbali za kiuchumi ili kurahisisha maisha yao na kupunguza changamoto za ajira kwa vijana nchini.
