Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MADIWANI BARIADI MJI WALIA UHABA WA DAWA ZA PAMBA.

MADIWANI BARIADI MJI WALIA UHABA WA DAWA ZA PAMBA.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Nkenyenge Charles (katikati) akiwa kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Nyaumata, kulia ni Makamu Mwenyekiti Zawadi  Mkilila na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Judith Ringia.


Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.

MADIWANI wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu, wameitaka Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), kuhakikisha inasambaza kwa wakati pembejeo za dawa ili wakulima waweze kudhibiti wadudu wanaoshambulia zao hilo. 


Aidha Madiwani hao wameiomba serikali kuangalia upya mfumo wa mnunuzi mmoja wa Pamba kwenye kijiji au mtaa jambo ambalo linawaondolea wakulima hao ushindani wa bei.


Wakizungumza kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani cha kujadili taarifa za robo ya pili 2025/2026, kilichofanyika ukumbi wa Nyaumata Madiwani hao walisema kuwa dawa zilizoletwa na serikali haziwatoshi wakulima, Hivyo Bodi ya Pamba wanapaswa kupeleka pembejeo hizo muhimu kwa Wakulima. 


Martine Singibala, Diwani wa Kata ya Mhango amesema wakulima wamelima na kupanda Pamba japo kwa kusuasua, sasa wanahitaji kupata dawa lakini hazipatikani, hivyo wanalalamika dawa hakuna katika maeneo yao.

Martine Singibala, Diwani wa Kata ya Mhango akitoa hoja kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani.


"Pamba iko kwenye hatua ya kubeba vitumba, wadudu wanaoshambulia ni wengi, ni lini serikali kupitia TCB itafikisha dawa kwa wakati kwa wakulima..." Alihoji Diwani huyo.



Diwani wa Kata ya Somanda, Majaba Malase, amesema kuwa dawa zilizosambazwa na serikali zimeletwa bila muda wa kutengenezwa wala muda wa kuisha matumizi, jambo linalowafanya wakulima washindwe kuamini kama zitauwa wadudu.



"Anayehudumia kata yangu ana majibu ya ovyo, tukikubali hili hatuwezi kuwasaidia wananchi, lazima tuondoke na maadhimio ili kuishauri serikali...Dawa zilizoletwa hazitoshi, tunaomba watuongezee dawa za Pamba pia watuleteee takwimu sahihi za dawa na mashamba ya wakulima ili kuondoa migogoro hiyo." Amesema Majaba. 


Diwani wa Kata ya Somanda, Majaba Malase (kulia) akichangia hoja kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani.


Lugembe Gichalu, Diwani wa Malambo, amesema mfumo wa mnunuzi mmoja ni sawa na unyonyaji wa zao la pamba kwa Wakulima, huku akisisitiza kuwa zao la pamba katika Mkoa wa Simiyu ndio zao la biashara na endapo watu hawatalims Pamba mapato ya serikali yatapungua.


Diwani wa Viti Maalumu, Spora Edward (kushoto) akichangia hoja kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani.


Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Nkenyenge Charles, ameiomba serikali kuangalia upya mfumo wa Kata moja kupewa mununuzi mmoja, kwani akipata changamoto ya fedha, wakulima wanakosa huduma ya fedha wakati huo wameuza Pamba yao.


"Tuweke azimio kama baraza, Kilimo ni Biashara, Tunapoteza maana ya ushindani kwenye soko sababu ya mnunuzi mmoja, huu mfumo tunauona unadidimiza mkulima, tutaona kwenye uzalishaji na je mkulima anarudisha gharama za uzalishaji?...Madiwani tuna haja ya kuangalia eneo hili, tujue mfumo wa Maafisa ugani wa BBT sababu tunasokia BBT analipwa kulingana na jasho la mkulima." Amesema na kuongeza.


"Huu mfumo wa Wafanyabiashara wa Pamba kununua Pamba kwenye kata moja ni mfumo gandamizi, tunaona tija ya kuwa na makampuni mengi, hapa mkulima anakosa nguvu ya kulima Pamba sababu ya Bei, Madiwani tunaomba ununuzi wa Pamba kwa mnunuzi mmoja wafanye mabadiliko."


Ameongeza kuwa Mkulima akikosa fedha hawezi kusubiri mpaka mfanyabiasha apate fedha, jambo ambalo siyo zuri wa wakulima na kwamba paamba nyingi inauzwa kwenye Halmashauri zingine na kuwakosesha mapato.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Nkenyenge Charles akiongea kwenye kikao cha Baraza la Madiwani 


Akijibu hoja hizo, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Slvanus Gwiboha amesema Serikali inaendelea kutoa pembejeo kwa wakulima kwaawamu kupitia mfumo wa ruzuku ambapo kila mkulima amesajiliwa kwa namba ya Nida na simu ya mkononi ili iwe rahisi kumfuatilia.


" Mbegu sasa zinatolewa kwa mfumo wa ruzuku, kutokana na mvua kuchelewa wakulima walichelewa kupanda, tumpewa chupa za dawa 25,000 lakini hazikutosha, tumetuma maombi na wiki hii tunaweza kupata dawa..Maafisa ugani wa BBT ni mfumo wa ushirikiano wa serikali na Kampuni zinazonunua Pamba ili kuongeza ushirikiano wa uzalishaji wa Pamba, wanalipwa na Kampuni kupitia gharama za Uendeshaji" amesema Gwiboha 


Ameeleza kuwa katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi kuna vijana wa BBT 23 ambao wamefanya kazi ya kutembelea wakulima na kuwaelimisha kuongeza uzalishaji wenye tija na kwamba serikali kupitia sekta binafis imeweza kuongeza ajira kwa Vijana.


Mwisho. 


Wataalamu wa Halmashauri wakiwa kwenye Kikao.



Madiwani wakiwa kwenye Kikao cha Baraza.










Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3