MADIWANI WAIOMBA SERIKALI KUKIDHIBITI KIWANDA CHA TRIWIN KUTIRIRISHA MAJI MACHAFU.
Feb 12, 2026
Kiwanda cha Triwin Agricultural Resources (T) Ltd kilichopo Kata ya Isanga, Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.
Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu limelitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kukitembelea na kukikagua kiwanda cha Triwin Agricultural Resource (T) Ltd kilichopo kata ya Isanga ambacho kinasadikiwa kutitirisha maji machafu kuelekea kwenye mashamba na makazi ya Wananchi.
Aidha Madiwani hao wameitaka serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kufanya tathimini ya athari za Mazingira zilizosababishwa na kiwanda hicho ili kuwalipa fidia wananchi ambao wameharibiwa mazao yao ambayo yameunguzwa na Maji hayo yanayosadikiwa kuwa na sumu.
Wakizungumza juzi kwenye Kikao cha kujadili taarifa za Maendeleo ya kata, robo ya pili 2025/2026, Madiwani hao walisema Kiwanda hicho kinatitirisha Maji machafu kuelekea kwenye makazi na mashamba ya watu ambayo yameanza kuleta adha ikiwemo mimea kukauka.
Diwani wa Kata ya Isanga, Nashon Ngusa aliliomba Baraza la Madiwani kumuunga mkono ili jambo hilo liweze kutatua jambo hilo huku akifafanua kuwa mpaka sasa wananchi hawajui mkataba wa kiwanda hicho na serikali.
Zao la Mpunga likiwa limeathiriwa na Maji yanayosadikiwa kuwa na sumu kutoka kwenye kiwanda cha Triwin kilichopo Kata ya Isanga, Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu .
Awali Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Monica Deusdedith alisema wameshatembelea kiwanda hicho na kukutana na wasaidizi ambao walidai kuwa kiwanda hicho hakifanyi kazi yoyote.
"Tulikuwa kiwanda kinaunguruma, walisema kiwanda kinafanyiwa matengenezo, tulikagua na kukuta Maji machafu yanavuja kwenye ukuta na Kuna bomba linatoa Maji machafu, Tulikuta Maji yametuama na kutengeneza bwawa pia tuliona kuna majaruba yamezungurwa na Maji...tumewaandikia barua walipe faini kulingana na Sheria zetu na tumemtaka achukue sampuli ili kupima Maji hayo na wawalipe fidia huyo wananchi hao" alisema.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Judith Ringia alitoa pole kwa wananchi wa Kata ya Isanga kwani kutitirisha maji, si ruhusa kwa Mwekezaji kwenda kwenye mashamba au makazi ya Wananchi.
Alisema kuwa wanafuatlia suala hilo kwa kuchukua sampuli ili kuzipeleka kwa Mkemia Mkuu wa serikali pamoja na kufuatilia ili hatua sahihi ziweze kuchukuliwa.
Sehemu ya mtaro ukiwa umezibwa ambao ulikuwa unatumika kutiririsha Maji machafu kutoka kiwanda cha Triwin kilichopo Kata ya Isanga, Halmashuri ya Mji wa Bariadi.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Nkenyenge Charles alisema Kiwanda hicho kinatitirisha Maji taka kwenda kwenye makazi ya wananchi na hatujui kama yana sumu au laa?..
"Watu wa Idara ya Mazingira wapo, wataalam tusaidieni sheria zikoje?.. tunataka tujue Nemc imekuja ikatoa maelekezo gani pale. ??" Alihoji Mwenyekiti huyo Nkenyenge na kuongeza.
Aidha, Nkenyenge alimtaka Afisa Mazingira kuwa mwadilifu na suala hilo kwani hawezi kumwelekeza achukue sampuli akapime mwenyewe halafu atoe majawabu.
Waandishi wa Habari walifika kiwandani hapo na kukuta greda zikichimba na kufukia sehemu ya mitaro iliyokuwa inatiririsha Maji hayo kwenda kwenye mashamba ya wananchi.
Jitihada za kuupata uongozi wa kiwanda hicho uligonga mwamba baada ya kumkuta getini mlinzi aliyejitambulisha kwa jina moja la Salum na kudai kuwa wahusika hawapo na pia kiwanda hakifanyi shughuli yoyote kwa Sasa.
Mwisho.
Majani yakiwa yamekauka kutokana na kutiririshiwa Maji yanayosadikiwa kuwa na sumu kutoka kiwanda cha Triwin kilichopo Kata ya Isanga, Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.

















