Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
FAIDA ZA VIJANA KUJIAJIRI WENYEWE

FAIDA ZA VIJANA KUJIAJIRI WENYEWE

 



Na Catherin Kilwale (UoI), Matukio Daima Media

Wakati changamoto ya ajira ikiendelea kuwa kikwazo kwa vijana wengi, hususan wahitimu wa vyuo vikuu, vijana wa Mtaa wa Semtema, Kata ya Kihesa mkoani Iringa, wameamua kujiajiri na sasa wanashuhudia matokeo chanya ya juhudi zao.

Vijana hao wanasema kujiajiri kumewasaidia kujitegemea kiuchumi, kupunguza utegemezi kwa familia na kuchangia maendeleo ya jamii inayowazunguka.

Akizungumza na Matukio Daima Media, Stephano Honga, mkazi wa Semtema anayejishughulisha na ufundi seremala, alisema ujasiriamali umemuwezesha kukidhi mahitaji yake ya kila siku pamoja na kuihudumia familia yake.

“Naweza kugharamia mahitaji yangu na ya familia yangu. Faida kubwa ni kwamba nasomesha watoto wangu kupitia kazi hii. Pia najiongoza mwenyewe bila kusimamiwa na mtu mwingine,” alisema Honga.

Aliongeza kuwa kujiajiri kumempa uhuru wa kupanga ratiba yake ya kazi na kuongeza kipato kulingana na juhudi na ubunifu wake.



Kwa upande wake, Grace Bayo, mjasiriamali wa eneo hilo, aliwahimiza vijana wanaokaa mtaani bila shughuli rasmi kuacha kukata tamaa na kuanza kutumia fursa zilizopo kwa maendeleo yao.


“Sio lazima kuanza na mtaji mkubwa. Ukiwa na nia na jitihada unaweza kufanikiwa. Changamoto zipo, lakini kikubwa ni kuwa na dhamira na matumaini,” alisema Grace.

Naye Majaliwa Mashaka, anayejishughulisha na uchomeleaji vyuma, alisema ukosefu wa ajira unapaswa kuwa chachu ya vijana kujitafutia ajira badala ya kusubiri kuajiriwa.


“Kujiajiri kunatufanya tusitegemee wengine na kutokuwa mzigo kwa familia. Pia tunaweza kusaidia wenye uhitaji na kuwashauri vijana wengine waanze kujishughulisha. Mafanikio hayaji kwa kukaa nyumbani bila kufanya kazi,” alisema Majaliwa.

Vijana hao wamewataka wenzao kubadili mtazamo kuhusu ajira na kuona ujasiriamali kama fursa ya kujikwamua kiuchumi, badala ya kusubiri ajira rasmi ambazo ni chache.

Kwa ujumla, wamesisitiza kuwa kujiajiri ni njia mojawapo ya kupambana na ukosefu wa ajira na kujenga jamii yenye vijana wanaojitegemea na kuchangia maendeleo ya taifa.



Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3