KUPANDA BEI YA MASWETA MKOA WA IRINGA
Na Ester Sebastian (UOI), Matukio Daima Media
WAFANYA biashara mkoani Iringa wameelezea sababu za kupanda kwa bei ya masweta wakati wa msimu wa masika, wakitaja changamoto za usafirishaji wa mizigo kuwa chanzo kikuu cha ongezeko hilo.
Wakizungumza na Matukio Daima Media kwa nyakati tofauti, wafanyabiashara hao walisema kipindi cha mvua huambatana na gharama kubwa za usafiri hali inayosababisha bei za bidhaa kupanda, ikiwemo masweta ambayo huhitajika zaidi wakati wa baridi.
Mfanyabiashara Jacob Daniel alisema kuwa msimu wa mvua huathiri biashara kwa kiasi kikubwa kutokana na kupanda kwa gharama za kusafirisha mizigo kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
“Katika msimu wa mvua tunakumbana na changamoto nyingi, ikiwemo gharama za usafirishaji kupanda. Hali hiyo husababisha bei ya masweta kuongezeka pia wakati mwingine wateja hupungua kwa sababu ya mvua, lakini mvua zinapokatika mahitaji huongezeka kwa kuwa wengi huhitaji masweta kwa wingi,” alisema Daniel.
Kwa upande wake, mfanyabiashara Marry Lilian alisema hukumbana na changamoto ya wateja kufika dukani kuulizia bei na kuondoka bila kununua kutokana na bei kuwa juu tofauti na matarajio yao.
Aidha, alieleza kuwa ucheleweshaji wa mizigo kufika dukani kwake wakati wa mvua huathiri upatikanaji wa bidhaa kwa wakati.
“Changamoto kubwa ni usafirishaji wa mizigo kuchelewa kufika. Wateja wanaagiza lakini bidhaa hazifiki kwa wakati, hali inayosababisha kukosa mauzo,” alisema Lilian.
Naye mteja wa masweta, Gasper Costantine, alisema kupanda kwa bei kunawaumiza wanunuzi hasa pale wanapokuta bei tofauti na matarajio yao.
“Unaweza kutoka nyumbani ukiwa na shilingi 25,000 ukitegemea kununua sweta, lakini ukifika dukani unakuta linauzwa shilingi 45,000 inakulazimu kurudi nyumbani kuchukua fedha zaidi, hivyo unaingia hasara ya nauli na muda,” alisema Costantine.
Hali hiyo imeibua mjadala miongoni mwa wakazi wa mkoa wa Iringa, wakiiomba mamlaka husika kufuatilia mwenendo wa bei ili kulinda maslahi ya walaji na wafanyabiashara kwa ujumla, hasa katika kipindi hiki cha masika.


