Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 HALMASHAURI YA MBEYA YAGAWA VISHIKWAMBI 40 KWA MADIWANI KUIMARISHA UTENDAJI KAZI

HALMASHAURI YA MBEYA YAGAWA VISHIKWAMBI 40 KWA MADIWANI KUIMARISHA UTENDAJI KAZI


Na Samwel Mpogole - Mbeya.

Jumla ya vishikwambi 40 vimetolewa kwa madiwani wa Halmashauri ya Mbeya kwa lengo la kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao, kuongeza ufanisi katika usimamizi wa shughuli za maendeleo pamoja na kuimarisha mawasiliano na upatikanaji wa taarifa muhimu za kiutendaji. 


Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani, Aidda Haule, amewataka madiwani hao kuhakikisha wanavitumia vishikwambi hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa, ikiwemo kusoma na kupitia nyaraka za vikao kwa wakati, kufuatilia miradi ya maendeleo katika kata zao pamoja na kusimamia ukusanyaji wa mapato ya halmashauri.



Amesisitiza kuwa vifaa hivyo ni nyenzo ya kazi, hivyo ni wajibu wa kila diwani kuvitunza na kuvitumia kwa umakini ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wao, baadhi ya madiwani waliopokea vishikwambi hivyo wameishukuru halmashauri kwa kuwapatia vifaa hivyo wakieleza kuwa vitarahisisha utendaji wao wa kazi, kupunguza matumizi ya karatasi na kuongeza wepesi wa kupata taarifa muhimu wakati wa vikao na katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Wilaya, Devotha Chacha amewataka madiwani kuhakikisha wanahimiza wananchi kuchangia na kulipa mapato stahiki ya halmashauri ili kuongeza makusanyo ya ndani yatakayosaidia kugharamia miradi ya maendeleo na kuboresha huduma za kijamii.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Edson Nyabwela akimuwakilisha Meneja wa RUWASA, ameeleza utekelezaji wa miundombinu ya barabara katika Wilaya ya Mbeya kwa kipindi cha mwaka 2026/2027, akibainisha kuwa juhudi zinaendelea kufanyika kuboresha na kujenga barabara za vijijini ili kurahisisha usafirishaji wa mazao, huduma za kijamii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.


Amesema ushirikiano kati ya viongozi, watendaji na wananchi ni muhimu katika kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya kwa jamii.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3