Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
HUDUMA ZA KIBINGWA ZA UPASUAJI ZAWAPA MATUMAINI MAPYA WANANCHI MBEYA.

HUDUMA ZA KIBINGWA ZA UPASUAJI ZAWAPA MATUMAINI MAPYA WANANCHI MBEYA.

 




Na Samwel Mpogole - Mbeya


Katika juhudi za kuimarisha huduma za afya na kuwafikia wananchi Nyanda za Juu Kusini na Nchi za jirani, Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya imeendesha Kambi Maalumu ya matibabu ya Upasuaji wa goti na nyonga iliyogusa maisha ya wagonjwa wengi waliokuwa wakisumbuliwa na magonjwa ya mifupa na majeraha kwa muda mrefu.


Zaidi ya wagonjwa 615 fika kwa uchungizi na matibabu kupitia kambi hiyo wameeleza furaha na shukrani zao kwa Serikali pamoja na Madaktari bingwa waliofanikisha upasuaji huo.


Emmanuel Mwankeja, mwananchi kutoka Kyela, amesema kwa hisia kuwa alikuwa akiishi kwa maumivu makali kwa muda mrefu kabla ya kupata fursa ya kufanyiwa upasuaji kupitia kambi hiyo.


“Nilikuwa nateseka sana na kushindwa kufanya kazi zangu za kila siku. Kupitia kambi hii nimepata matibabu bure na sasa naona matumaini mapya ya maisha,” amesema Emmanuel.


Kwa upande wake, Thadei Kalokole, mkazi wa Iyunga, amesema kambi hiyo imekuwa mkombozi kwake baada ya kusumbuliwa na tatizo la muda mrefu bila mafanikio ya matibabu ya uhakika.


“Nilikuwa nimekata tamaa, lakini leo namshukuru Mungu na madaktari kwa kunirejeshea matumaini. Maumivu yamepungua na ninaendelea vizuri,” amesema Thadei.



Kwa upande wake, Dkt. Baraka Mponda, Bingwa wa Upasuaji wa Mifupa na Majeraha kutoka Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, amesema kambi hiyo imeongeza ufanisi wa utoaji huduma na kutoa fursa kwa wagonjwa waliokuwa kwenye orodha ya muda mrefu kupata matibabu kwa wakati.


Akizungumzia mafanikio ya kambi hiyo, Profesa Billy Haonga, Daktari Bingwa Mshauri wa Upasuaji wa Mifupa na Majeraha kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, amesema lengo la kambi hiyo ni kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi na kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaolazimika kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu.


Ameeleza kuwa timu ya madaktari bingwa imefanikiwa kufanya upasuaji kwa wagonjwa wengi waliokuwa na changamoto mbalimbali za mifupa na majeraha, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza kambi kama hizo mara kwa mara.



Naye Dkt. Joseph Mjemvua ameishukuru serikali na uongozi wa hospitali kwa kuwezesha upatikanaji wa vifaa tiba na ushirikiano wa wataalamu uliowezesha mafanikio ya kambi hiyo.


Kambi hiyo imeonekana kuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Mbeya na mikoa jirani, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali za kuboresha sekta ya afya na kuhakikisha huduma za kibingwa zinawafikia wananchi kwa wakati na ubora unaostahili.


Kwa ujumla, wananchi wameendelea kutoa pongezi kwa uongozi wa hospitali na madaktari wote waliohusika, wakisema kambi hiyo imekuwa chachu ya matumaini mapya na faraja kwa wengi waliokuwa wakiishi katika maumivu kwa muda mrefu.


Huduma iyo ya matibabu ya kibingwa bobezi sasa inatolewa na hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kwa ufanisi mkubwa kusaidia wananchi kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu ndani na nje ya nchi.


Mwisho.







Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3