EWURA: MALALAMIKO YA WANANCHI YATATULIWA BURE, WAANDISHI WATUMIKE KUELIMISHA UMMA
Feb 27, 2026
Matukio Daima, Dar es salaam.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesisitiza kuwa huduma ya utatuzi wa migogoro kati ya wateja na watoa huduma hutolewa bila gharama yoyote kwa wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika mkutano wa tathmini wa utendaji kazi yaliyoandaliwa na MISA Tanzania, Meneja wa EWURA Kanda ya Mashariki, Mhandisi Lorivii Long’idu, amesema wananchi wanapaswa kujitokeza kuwasilisha malalamiko yao badala ya kunung'unika.
Ametoa mfano wa changamoto za mafuta yasiyo na ubora, bili pandikizi za maji na umeme, akisisitiza kuwa EWURA hufanya uchunguzi kwa gharama zake hadi haki itendeke.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Mawasiliano wa EWURA, Willfred Mwakalosi, amezitaka taasisi zinazodhibitiwa na mamlaka hiyo kuweka wazi mikataba ya huduma kwa wateja.
Amesema uwazi huo utawawezesha wananchi kufahamu haki na wajibu wao na kupunguza migogoro isiyo ya lazima.
Naye Mwenyekiti wa MISA TAN, Edwin Soko, amesema vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kuelimisha jamii kuhusu masuala muhimu yakiwemo ya nishati na maji.
Ameeleza kuwa ushirikiano kati ya EWURA na MISA TAN umeongeza ubora wa habari na kusaidia wananchi kupata taarifa sahihi kwa wakati.



