Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
AJALI YA BASI LINDI YAUA WAWILI, 12 WAJERUHIWA

AJALI YA BASI LINDI YAUA WAWILI, 12 WAJERUHIWA

NA MATUKIO DAIMA MEDIA LINDI

Watu wawili wamefariki dunia huku wengine 12 wakijeruhiwa kufuatia ajali ya basi la kampuni ya Maning Nice lililokuwa likitokea Jijini Dar es Salaam kuelekea Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, baada ya kugonga lori lililokuwa limeharibika katika eneo la Mtange, barabara ya Lindi – Mnazi Mmoja.

Kwa mujibu wa mashuhuda wamesema ajali hiyo imetokea majira ya saa 12 asubuhi, ambapo miongoni mwa waliofariki ni mwanaume mwenye umri wa miaka 50 na mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Februari 7, 2026, Muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, Ofisa Yusuph Salim, amesema hospitali hiyo ilipokea miili ya marehemu wawili pamoja na majeruhi 12 majira ya saa 1:15 asubuhi.

Amesema kati ya majeruhi hao, wawili wamepelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi, huku majeruhi 10 wakiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi.


“Tumepokea miili miwili, mmoja ni mwanaume mwenye umri wa miaka 50 na mtoto wa mwaka mmoja na nusu, pamoja na majeruhi 12. Miili imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti, majeruhi 10 wanaendelea na matibabu na wawili wamepelekwa Hospitali ya Muhimbili,” amesema Salim.

Kwa upande wake, mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, Rajabu Masoud, mkazi wa Kigamboni Jijini Dar es Salaam, amewataka madereva kuwa wanasaidiana katika kuendesha magari ili kupunguza ajali za barabarani.

Masoud amesema kuwa walipofika Lindi, alimsikia dereva wa basi hilo akimwambia dereva mwenzake kwamba wakifika Mnazi Mmoja angemkabidhi usukani, lakini hawakufanikiwa kufika eneo hilo kabla ya kupata ajali.

Jitihada za kumtafuta kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi bado zinaendelea

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3