MADIWANI KIGOMA UJIJI WACHARUKA BARABARA KUKWAMISHA SHUGHULI ZA UCHUMI
Mkurugenzi wa manispaa ya Kigoma Ujiji Kisena Mabuba (kulia) akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani la Kigoma Ujiji juzi (katikati) ni Meya wa manispaa hiyo Mussa Maulid na (kushoto) Naibu Meya Mgeni Kakolwa
Meya wa manispaa ya Kigoma Ujiji Mussa Maulid (katkati) akifunga kikao cha baraza la madiwani la manispaa ya Kigoma Ujiji juzi (kushoto) Naibu Meya Mgeni Kakolwa na (kulia) Mkurugenzi wa manispaa ya Kigoma Ujiji Kisena Mabuba.
Madiwani wa manispaa ya Kigoma Ujiji wakiwa kwenye kikao cha baraza
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Madiwani katika halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji wameitaka wakala wa barabara za mijini na vijijini (TARURA) kuboresha barabaraa za manispaa hiyo na kujengwa kwa kiwango cha lami ili kuchochea shughuli za biashara na uchumi za wananchi wa manispaa hiyo.
Diwani wa kata ya Businde Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma, Masudi Kassim akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani alisema kuwa barabara nyingi ambazo zilijengwa kwa kiwango cha changarawe zimeharibika kwa mvua na sasa hali ya usafirishaji bidhaa ni ngumu na gharama kubwa hivyo TARURA ifanye jitihada kuhakikisha barabara hizo zinarekebishwa
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Buhanda, Edward Misigaro, alisema baadhi ya miradi ya barabara inayotekelezwa kwa awamu imechukua muda mrefu kukamilika ukiwemo mradi wa uboreshaji wa miundo mbinu ya miji (TACTIC) kwa kiwango cha lami hivyo kusababisha kutofanyika kwa miradi mingine jambo linaloendelea kuwaumiza wananchi.
Akizungumzia kauli za madiwani katika kikao hicho, Meneja wa TARURA Wilaya ya Kigoma, Elias Mtapima, alisema asilimia kubwa ya barabara za mitaa katika manispaa hiyo zinahitaji maboresho makubwa, lakini changamoto kubwa inayokabili utekelezaji wa miradi hiyo ni ukomo wa bajeti.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Kisena Mabuba, alisema juhudi zinaendelea kufanyika katika kuandaa maandiko ya miradi mbalimbali ya miundombinu, ikiwemo barabara na mifereji ya maji ya mvua ili kuhakikisha manispaa hiyo inapata ufadhili wa kutosha kwa ajili ya utekelezaji wake.


