WAZIRI MKUU KUZINDUA RASMI MELI YA MV NEW MWANZA JIJINI MWANZA.
Jan 22, 2026
NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kuzindua rasmi Meli ya MV New Mwanza kesho tarehe 23 Januari, 2026, katika Bandari ya Mwanza Kusini, Jijini Mwanza iliyogharimu zaidi ya Sh, Bil 120.
Akizungumza na waandishi wa habari Waziri wa Uchukuzi, Prof Makame Mbarawa, ameeleza kuwa Meli ya MV New Mwanza ni meli kubwa kuliko zote katika Ziwa Victoria na ina uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari makubwa 3 na magari madogo 20.
Waziri Mbarawa alisema ujenzi wa meli hiyo ulitekelezwa kwa mkataba kati ya Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) na Kampuni ya GAS Entec Company Limited kwa kushirikiana na KANGNAM Corporation kutoka Korea ya Kusini pamoja na SUMA JKT ya Tanzania, chini ya usimamizi wa Kampuni ya OSK Shiptech kutoka Denmark.
Ameeleza kuwa meli hiyo iliyoshushwa majini rasmi tarehe 12 Februari, 2023 baada ya kukamilika kwa ujenzi wa umbo la meli na kufungwa kwa baadhi ya mifumo muhimu na baada ya kukamilika kwa ujenzi, meli ya MV New Mwanza ilifanya safari za majaribio kuanzia tarehe 15 hadi 17 Machi, 2024.
" Hatua hiyo iliruhusu kuendelea kwa kazi nyingine za ujenzi meli ikiwa tayari iko majini na wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaingia madarakani, mradi huo ulikuwa umefikia asilimia 40 ya utekelezaji, huku mkandarasi akiwa amelipwa Shilingi 40,644,775,180.03" Alisema Mbarawa.
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ilitoa fedha zilizohitajika kukamilisha mradi huo, na hadi sasa mkandarasi amelipwa asilimia 98 ya fedha zote.
Ameeleza kuwa baada ya kukaguliwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), meli iliruhusiwa kuanza safari za kibiashara na hadi sasa imefanya safari sita kati ya Mwanza na Bukoba kupitia Kemondo, ikibeba abiria 7,028 na kusafirisha takribani tani 673 za mizigo.
Waziri Mbarawa alisema kufanyika kwa safari hizo ni uthibitisho wa kukamilika kwa ujenzi wa Meli ya MV New Mwanza na kuwa meli hiyo ipo katika ubora uliosanifiwa na ni salama kwa usafiri wa abiria na mizigo majini, hivyo Serikali imeona ni wakati muafaka wa kufanya uzinduzi rasmi wa meli hiyo.
Aidha amewata wananchi wa Jiji la Mwanza na viunga vyake pamoja na Mikoa ya Kanda ya Ziwa wanakaribishwa kushiriki na kufuatilia uzinduzi wa Meli ya MV New Mwanza katika Bandari ya Mwanza Kusini.



