Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WAZIRI MAVUNDE AAGIZA KUFUTWA LESENI ZISIZOFANYIWA KAZI

WAZIRI MAVUNDE AAGIZA KUFUTWA LESENI ZISIZOFANYIWA KAZI

Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, amewaagiza Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa yote nchini kuwasilisha ndani ya siku saba orodha ya leseni za uchimbaji madini ambazo hazifanyiwi kazi, akisema leseni zote zitakazobainika kutofanyiwa kazi zitafutwa mara moja kwa mujibu wa sheria.

Mavunde ametoa maagizo hayo leo Januari 22,2016 Jijini Dodoma alipokuwa akizungumza katika Kikao cha Menejimenti ya Tume ya Madini cha robo ya pili, akisisitiza kuwa Serikali haitaendelea kuvumilia hali ya watu kumiliki leseni kwa ajili ya kuzifungia bila kuendeleza shughuli za uchimbaji.

Amesema lengo la hatua hiyo ni kuongeza uzalishaji katika sekta ya madini na kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha Watanzania wengi zaidi kupitia ajira, mapato ya Serikali na maendeleo ya maeneo yenye madini.


Waziri huyo pia aliwataka Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya baadhi ya Maofisa wa chini ambao wamekuwa wakichafua ofisi zao kwa kujihusisha na vitendo vya kujimilikisha au kutoa leseni za uchimbaji kwenye maeneo ambayo tayari yana wachimbaji halali, hali inayosababisha migogoro isiyo ya lazima.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Madini nchini, Janeth Lekashingo, alisema kuwa katika kipindi cha nusu ya Mwaka wa Fedha 2025/2026, Tume hiyo imekusanya jumla ya Shilingi bilioni 663.94, ikiwa ni ongezeko la asilimia 25.39 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka wa fedha uliopita.


Lekashingo amesema ongezeko hilo linatokana na kuimarika kwa usimamizi wa shughuli za madini, kuongezeka kwa uzalishaji pamoja na maboresho katika ukusanyaji wa maduhuli.


Katika kikao hicho, Waziri Mavunde pia amekabidhi jumla ya magari 23 kwa Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa, hatua inayolenga kuboresha usimamizi wa shughuli za uchimbaji madini na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika mikoa mbalimbali nchini.


MWISHO

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3