DC THOMAS MYINGA:WAJAWAZITO WANAOTUMIA DAWA ZA KIENYEJI KUTOZWA FAINI
Na Linah Rwamba
Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Thomas Myinga amemwelekeza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Seif Salum kusimamia uwajibishaji wa mama wajawazito wanaotumia dawa za asili kuongeza uchungu kwasababu kitendo hiko hupelekea athari kwa mama na mtoto.
Myinga ameyasema hayo wakati akizungumza na Timu ya Uendeshaji Huduma za Afya Wilaya na Waganga Wafawidhi katika Ukumbi wa Hospitali ya Wilaya.
"Nitoe maelekezo kwako Mkurugenzi kuwatumia Watendaji wa Kata kuelimisha na kutoza faini wajawazito wote watakaokunywa dawa za asili kwaajili ya kuongeza uchungu ili kuepuka vifo vya mama au matatizo ya upumuaji kwa watoto watakozaliwa kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa Wilaya, Dokta Esther Kayamba" amesema.
"Mama akija Hospitali akiwa amekunywa dawa hizo, muhudumieni kisha akikaa sawa wewe daktari uliyempokea piga simu kwa Mtendaji ili atozwe faini kwa kosa hilo" amesema Myinga.
Aidha Myinga amewaagiza wahudumu wa afya kusikiliza wagonjwa vizuri ili waweze kutoa huduma stahiki.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Ndg. Seif Salum amepokea maelekezo hayo na kuwataka waganga wafawidhi kuzingatia asilimia 35/50 iliyotengwa kwaajili ya dawa itumike ipasavyo kwasababu wakifanya hivyo changamoto ya dawa itaisha.

