AZIZ KI ABWAGA MANYANGA WYDAD ATUA HUKU ...
Jan 21, 2026
Hatimaye kiungo Stephane Aziz Ki ameachana na Wydad AC ya Morocco na kujiunga na Al Ittihad ya Libya kwa mkataba wa miaka miwili.
Aziz Ki ambaye alijiunga na Wydad, Mei mwaka jana, ameachana na Wydad baada ya kuitumikia timu hiyo kwa muda wa miezi nane tu tangu alipojiunga nayo kutokea Yanga.
Usajili wa nyota wa zamani wa Sevilla na timu ya Taifa ya Ufaransa, Wissam Ben Yedder ambao Wydad itaukamilisha hivi karibuni, unaonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa kuishawishi klabu hiyo kumfungulia mlango wa kutokea Aziz Ki.
Inaripotiwa kuwa Al Ittihad imelazimika kulipa kitita cha Dola 300,000 ili kuipata saini ya kiungo huyo anayeichezea pia timu ya taifa ya Burkina Faso.
Al Ittihad imeonekana kuzizidi kete, MC Alger na Kaizer Chiefs ambazo pia zilikuwa zikimuwania kiungo huyo mshambuliaji mwenye umri wa miaka 29.
