WAHITIMU WA CHUO CHA MIPANGO WATAKIWA KUWA WABUNIFU, WAAJIRI WENGINE
Nov 21, 2026
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media, Dodoma
WAHITIMU wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini wametakiwa kutumia taaluma walizozipata kuanzisha miradi ya kiuchumi, kujiajiri na kutoa ajira kwa wengine ili kuongeza mchango wao katika ukuaji wa uchumi wa Taifa, badala ya kusubiri nafasi za ajira katika taasisi za umma na binafsi.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Deogratius Luswetula, ameyesisitiza kuwa elimu ya wahitimu inapaswa kuwa chachu ya kutengeneza fursa mpya za kiuchumi na kutatua changamoto zinazozikabili jamii.
Luswetula ametoa wito huo kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), wakati wa Mahafali ya 40 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Julius K. Nyerere, Kampasi Kuu ya Dodoma.
Amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira yanayowezesha wananchi, hususan vijana, kupata elimu, mitaji, teknolojia na masoko ili waweze kutumia uwezo wao kushiriki katika shughuli za uzalishaji na kukuza uchumi.
Amesema wahitimu wanapaswa kuachana na mtazamo wa kuona ajira za kuajiriwa kuwa ndiyo njia pekee ya kutumia elimu yao, badala yake wajikite katika kubuni fursa zinazoweza kuwapatia kipato na kuajiri wengine.
“Wahitimu wanapaswa kutumia maarifa na ujuzi walioupata kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za kiuchumi na kijamii, kwa kubuni fursa za kujiajiri na kuajiri wengine,” amesema Luswetula.
Katika kuwawezesha vijana kufikia malengo hayo, amesema Serikali imeongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kutoka Sh bilioni 916.7 mwaka wa fedha 2025/2026 hadi Sh trilioni 1.06 kwa mwaka 2026/2027, ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.6.
Amesema ongezeko hilo linatarajiwa kuongeza idadi ya wanufaika wa mikopo hiyo kutoka wanafunzi 252,773 hadi 289,932, hatua inayolenga kupanua fursa za upatikanaji wa elimu ya juu nchini.
Aidha, amesema Serikali imetenga Sh bilioni 9.6 kupitia Samia Scholarship kwa ajili ya wanafunzi 2,738 wanaosomea fani za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Tiba, huku Sh bilioni 200 zikitengwa kwa Programu ya Kitaifa ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi kwa lengo la kukuza ujasiriamali na kuongeza ajira.
Amefafanua kuwa jitihada nyingine ni kuendelea kutekeleza utaratibu wa kutenga asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri kwa ajili ya mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, sambamba na kutoa asilimia 30 ya manunuzi ya umma kwa makundi hayo.
Akizungumzia nafasi ya vyuo katika kukuza ujasiriamali, Luswetula alikipongeza Chuo hicho kwa kuanzisha Kituo cha Ujasiriamali na Ubunifu (MEI), kinacholenga kuwajengea wanafunzi uwezo wa kubadilisha mawazo yao kuwa bidhaa na huduma zinazoweza kuuzwa na kuleta manufaa kiuchumi.
Amesema kituo hicho ni daraja muhimu kati ya elimu inayotolewa chuoni na mahitaji ya soko, kwa kuwa kinawapa wanafunzi nafasi ya kukuza mawazo bunifu, kuanzisha biashara na hatimaye kujenga ajira.
“Ninapenda kukipongeza Chuo kupitia Kituo chake cha Ujasiriamali na Ubunifu (Mipango Entrepreneurship and Innovation Centre) kwa jitihada kubwa za kukuza ubunifu, ujasiriamali na kuwawezesha vijana kubuni na kuendeleza mawazo bunifu yenye uwezo wa kuunda bidhaa na huduma mpya,” amesema.
Aliongeza kuwa Serikali inaunga mkono mpango wa Chuo hicho wa kufungua Kituo cha Mafunzo katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini mkoani Songwe, hatua itakayosaidia kusogeza huduma za elimu karibu na wananchi na kupanua wigo wa upatikanaji wa mafunzo.
Amewataka wahitimu kuzingatia maadili, nidhamu na uwajibikaji katika maeneo yao ya kazi na shughuli za ujasiriamali, huku wakijijengea utamaduni wa kujifunza na kutumia maarifa yao kutatua changamoto za maendeleo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Profesa Mayaya, amesema jumla ya wanafunzi 6,076, wakiwemo wanaume 2,741 na wanawake 3,335, wamehitimu katika mahafali hayo kupitia programu mbalimbali za elimu kuanzia Astashahada ya Msingi hadi Shahada ya Uzamili.
Amesema maandalizi ya wahitimu hao yalihusisha mafunzo ya nadharia na vitendo, tafiti, mafunzo kazini pamoja na ushirikishwaji wa jamii, ili kuhakikisha wanapata maarifa yanayoweza kutumika katika kukabiliana na changamoto halisi za maendeleo.
Profesa Mayaya aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kuendelea kusaidia kuboresha miundombinu ya Chuo, akitaja kukamilika kwa Jengo la Taaluma lenye ghorofa nne lililojengwa kupitia Mradi wa HEET na lenye uwezo wa kuhudumia watu 1,628 kwa wakati mmoja.
Amesema Serikali pia inaendelea kufadhili ujenzi wa mabweni mawili, kila moja likiwa na uwezo wa kulaza wanafunzi 320, moja likiwa katika Kampasi ya Miyuji, Dodoma, na jingine katika Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa, Mwanza.
Alitaja Bweni Namba Nne linalojengwa eneo la Miyuji Kaskazini kuwa na thamani ya Sh bilioni 4.18 na uwezo wa kulaza wanafunzi 320, huku Bweni Namba Mbili linalojengwa katika Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa, eneo la Kisesa, Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, likiwa na thamani ya Sh bilioni 3.70 na uwezo kama huo.
Amesema ujenzi wa bweni la Kisesa umefikia hatua ya kupaua, akieleza kuwa miradi hiyo itasaidia kupunguza changamoto za malazi na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Katika eneo la ubunifu na ujasiriamali, Profesa Mayaya alisema Chuo kimefanikiwa kuwaendeleza wanafunzi 228 kupitia programu mbalimbali zilizolenga kuwajengea uwezo wa kuanzisha na kuendeleza shughuli za kibiashara.
Amesema miongoni mwa mafanikio hayo ni mwanafunzi mmoja kushika nafasi ya pili katika shindano la Bahari Innovation Challenge kupitia biashara ya Kalinga Fresh Fish Farm, ambapo alipata Sh milioni 29.8 pamoja na fursa nyingine za kibiashara.
Aidha, amesema Chuo kilipata Sh milioni 68 kupitia programu ya Youth Ignite ya FUNGUO chini ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), fedha zilizolenga kuboresha miundombinu ya kituo hicho cha ubunifu.
Amebainisha kuwa Chuo kitaendelea kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi, kufanya tafiti na kutoa huduma za ushauri elekezi katika masuala ya mipango na usimamizi wa maendeleo ili kuhakikisha taaluma zinazotolewa zinaendana na mahitaji ya jamii.
Mahafali hayo ya 40 yanaweka alama nyingine katika mchango wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini katika kuandaa wataalamu watakaoshiriki katika kupanga, kusimamia na kutekeleza shughuli za maendeleo, huku wakichangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi shindani, jumuishi na wenye tija kwa kupanua fursa za kiuchumi na ajira.
Mwisho.



