MVUA ZACHOCHEA ONGEZEKO LA MAJI MITO YA RUVU NA WAMI
Na Matukio Daima Media, Morogoro
Mvua zinazoendelea kunyesha katika safu za milima na maeneo ya vyanzo vya mito ya Ruvu na Wami zimeendelea kuchochea ongezeko la maji, huku hali ya sasa ikielezwa kuwa inatosheleza mahitaji ya watumiaji mbalimbali.
Taarifa ya Bodi ya Maji ya Bonde la Wami/Ruvu inaeleza kuwa Mto Ruvu umeendelea kunufaika na mvua za Milima ya Uluguru, ambapo kiwango cha maji katika eneo lililotajwa na Bodi kimefikia lita 16,700 kwa sekunde, na Ruvu chini kufikia lita 14,900 kwa sekunde.
Kwa upande wa Wami, mvua za milima ya Chenene, Nguu, Ukaguru na Rubeho zimeongeza kiwango cha maji hadi lita 9,700 kwa sekunde, hali inayowezesha kuendelea kukidhi mahitaji ya DAWASA, Bagamoyo Sugar Ltd na Hifadhi ya Taifa ya Saadani.
Matarajio ya siku 10 zijazo yanaonesha kuwa ongezeko la maji litaendelea katika mito yote miwili. Kwa Mto Ruvu, kiwango kinatarajiwa kuwa juu ya wastani wa muda mrefu wa miaka 2009 hadi 2024, huku Wami nao ukitarajiwa kuongezeka.
Pamoja na ongezeko hilo, taarifa ya Bodi iliyotolewa Novemba 20, 2026, haijaonesha viashiria vya tahadhari ya mafuriko katika maeneo mbalimbali ya mito ya Ruvu na Wami.
Bodi imeeleza kuwa itaendelea kufuatilia hali ya maji na kutoa taarifa za mara kwa mara pamoja na tahadhari kwa wadau kuhusu mabadiliko ya viwango vya maji, ikiwemo ongezeko au upungufu wake.