Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
TANZANIA YAFUNGUA MASOKO 10 YA KIMATAIFA KUPITIA KAMPENI YA CHANJO ZA MIFUGO

TANZANIA YAFUNGUA MASOKO 10 YA KIMATAIFA KUPITIA KAMPENI YA CHANJO ZA MIFUGO


Matukio Daima Media, Morogoro

Kampeni ya kitaifa ya chanjo na utambuzi wa mifugo imeanza kuimarisha nafasi ya Tanzania katika biashara ya kimataifa baada ya kufunguliwa kwa masoko mapya ya chanjo, nyama, mayai na wanyama hai, huku mauzo ya nyama nje ya nchi yakifikia tani 14,234 katika mwaka wa fedha 2025/2026.

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Benezeth Malinda, amesema mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji wa Serikali katika kudhibiti magonjwa ya mifugo na kuhakikisha bidhaa zinazouzwa nje zinakidhi masharti ya nchi zinazoagiza.

Amesema Tanzania imefungua masoko ya chanjo zinazozalishwa nchini katika nchi za Mongolia, Botswana, Ghana na Israel, nyama ya ng'ombe, mbuzi na kondoo pamoja na wanyama hai katika Mauritius, huku mayai yakipata masoko ya China, Sierra Leone, Ivory Coast, Ghana na Cameroon.

Dkt. Malinda ameeleza kuwa ongezeko la mauzo ya nyama linaonesha matokeo ya uwekezaji huo, ikilinganishwa na tani 669 zilizouzwa mwaka 2020, tani 1,770 mwaka 2021 na takribani tani 10,000 mwaka 2022. Serikali inalenga kufikisha mauzo hayo zaidi ya tani 50,000 ifikapo mwaka 2030.

Amesema Serikali ilizindua kampeni hiyo Juni 2025 kwa kipindi cha miaka mitano hadi 2030, ikiahidi kutumia Sh bilioni 216, ambapo Sh bilioni 62.2 zilitolewa katika mwaka wa fedha 2025/2026 na Sh bilioni 30.8 zimetengwa kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Fedha hizo zinagharamia ununuzi wa chanjo, heleni za kielektroniki za utambuzi, vifaa vya kuchanjia, ushiriki wa maofisa ugani wa halmashauri na vifaa vya kuhifadhia chanjo katika mazingira ya ubaridi.

Dkt. Malinda ameyasema hayo mjini Morogoro alipomwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena, katika hafla ya kufunga mafunzo ya ISAVET kwa madaktari na maofisa mifugo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Mtaalamu wa Afya ya Mifugo na Mratibu wa ISAVET kutoka FAO, Dkt. Moses Ole-Neselle, amesema mafunzo hayo yamejikita katika kuwawezesha wataalamu kutambua mapema magonjwa ya mifugo yanayoweza kuchangiwa na mabadiliko ya tabianchi, kufanya uchunguzi na utafiti pamoja na kutoa taarifa kwa wakati.

Mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) yamehusisha pia wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Zanzibar, wakiwemo Daktari Mkuu wa Mifugo Zanzibar, Dkt. Ali Zahran Mohamed, na Daktari wa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang'hwale, Suzana Joseph.

Pia yalihusisha ushiriki wa Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Daniel Mdetelo, katika mjadala wa kitaalamu kuhusu uimarishaji wa huduma za mifugo na udhibiti wa magonjwa.

Mwisho








 

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3