NDEGE WAHARIBIFU NA NZIGE WATISHIA UZALISHAJI WA CHAKULA AFRIKA MASHARIKI..
Nov 15, 2026
Matukio Daima Media, Morogoro
Uwezo wa ndege waharibifu aina ya kwelea kwelea na wadudu wanaohama, wakiwemo nzige wa jangwani na viwavi jeshi, kushambulia mazao kwa makundi makubwa unaendelea kuwa changamoto kwa uzalishaji wa chakula katika Afrika Mashariki. Hali hiyo inahitaji mifumo madhubuti ya kubaini mapema maeneo yaliyo katika hatari na kuchukua hatua za kudhibiti mashambulizi kabla hayajasababisha hasara kubwa kwa wakulima.
Wataalamu kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan Kusini na Ethiopia wamekutana mjini Morogoro katika mafunzo ya kikanda yanayolenga kuimarisha uwezo wa kutumia teknolojia ya anga kufanya uchunguzi, kufuatilia na kudhibiti ndege na wadudu hao kabla hawajasababisha hasara kubwa kwa wakulima.
Mafunzo hayo yanayoandaliwa na Shirika la Kudhibiti Nzige wa Jangwani katika Afrika Mashariki (Desert Locust Control Organization for Eastern Africa – DLCO-EA), kwa ushirikiano na Benki ya Waarabu kwa Maendeleo ya Kiuchumi Afrika (Arab Bank for Economic Development in Africa – BADEA), yamefanyika kwa muda wa siku nne mjini Morogoro.
Mkurugenzi wa DLCO-EA, Moses Mwesigwa, ameeleza mikakati mbalimbali ya shirika hilo katika kuimarisha udhibiti wa ndege na wadudu waharibifu, akieleza kuwa matumizi ya teknolojia za kisasa, ikiwemo ndege zisizo na rubani, ni miongoni mwa njia zinazoweza kutumika katika shughuli za udhibiti kwa kupulizia viuatilifu katika maeneo yaliyoathirika.
Meneja wa DLCO-EA upande wa Tanzania, Didas Moshi, anaeleza changamoto zinazojitokeza katika kudhibiti visumbufu hivyo na hatua zinazochukuliwa kukabiliana navyo, huku Meneja wa Usimamizi wa Visumbufu vya Mlipuko wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Godfrey Kirimbo, akieleza maeneo yenye changamoto zaidi na mikakati ya Serikali katika kukabiliana na mashambulizi hayo.
Mkutano huo pia unalenga kuimarisha ushirikiano wa nchi wanachama katika kubadilishana taarifa, utaalamu na teknolojia, kwa kutambua kuwa ndege na wadudu wanaohama hawazuiliwi na mipaka ya nchi moja, hivyo udhibiti wake unahitaji uratibu wa pamoja ili kulinda uzalishaji wa chakula, kipato cha wakulima na usalama wa chakula katika ukanda huo.
Mwisho




