SIKU SABA ZA KUREJESHA MVUHA, DC KILAKALA ATOA MAAGIZO KWA MCHIMBAJI
Matukio Daima Media, Morogoro
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, ametoa siku saba kwa mchimbaji wa madini, Omari Muhondogwa, kurejesha Mto Mvuha katika hali na mwelekeo wake wa asili baada ya kubainika kuharibiwa na shughuli za uchimbaji madini katika Kijiji cha Bungu.
Ametoa agizo hilo baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kufanya ziara ya kushtukiza na kubaini uchimbaji ndani ya eneo la hifadhi ya mita 60 kutoka kingo za mto, ukiambatana na mrundikano wa tope na kuvurugika kwa mfumo wa mtiririko wa maji.
Kilakala ameliagiza Jeshi la Polisi kumshikilia Muhondogwa kwa hatua za kisheria, huku Tume ya Madini ikitakiwa kusitisha leseni yake mara moja.
Pia amewataka wananchi waliopo ndani ya eneo la hifadhi kuondoka ili kupisha urejeshaji wa mto huo.
Hatua hizo zinatokana na umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji, hususan Mto Mvuha unaochangia asilimia 22 ya maji yanayoingia katika Bwawa la Kidunda.
Awali, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imetaka Mkoa wa Morogoro kuweka udhibiti wa uchimbaji holela katika mto huo baada ya kubaini uchimbaji madini na uchepushaji wa mkondo wa maji katika maeneo hayo yaliyopo kwenye Halmashauri ya wilaya ya Morogoro.
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Patrick Mwalunenge, na mjumbe Thomas Kampala, kwa nyakati tofauti wameeleza umuhimu wa kulinda chanzo hicho kwa usalama wa upatikanaji wa maji safi hasa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.



