Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 PROF.KITILA MKUMBO ATAKA  TANROADS  KUTUMIA UTU BOMOA BOMOA VIBANDA VYA BIASHARA

PROF.KITILA MKUMBO ATAKA TANROADS KUTUMIA UTU BOMOA BOMOA VIBANDA VYA BIASHARA


Na  Fadhili Abdallah,Kigoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo ameitaka Wakala wa barabara nchini (TANROADS) mkoa Kigoma kuzingatia utu na ubinadamu wanapotekeleza zoezi kuwaondoa wafanyabiashara wanaofanya biashara zao kando kando ya barabara zinazosimamiwa na wakala huo na kwamba zoezi hilo linasababisha umasikini mkubwa kwa Watanzania.

Waziri Mkumbo alisema hayo katika kongamano la siku moja na wafanyabiashara na wawekezaji wa mkoa Kigoma ambapo amepokea kilio na mmalalamiko makubwa ya wafanyabiashara ambao wamendolewa kwenye maeneo waliyokuwa wakifanya biashara huku wengine bidhaa zao zikiwa ndani na kwa sasa hawajui waende wapi.

Akizungumzia jambo hilo Profesa Kitila Mkumbo alisema kuwa amemka akiwa mkoani Kigoma amepokea simu kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo kutoka kwa wafanyabiashara na viongozi wa jimbo lake la Ubungo Dar es Salaam ambao wamevunjiwa mabanda yao na kuondolewa kwenye maeneo hayo huku wakiwa hawana pa kwenda na kwamba biashara hizo ndiyo msingi wa kuendesha familia zao.

“Tunajua zipo sheria na kauni ambazo zimetumika kutekeleza jambo hilo lakini pia kuna wakati utu na ubinadamu lazima uangaliwe kwani wananchi hao ni watanzania na serikali inawategemea kwa mambo mbalimbali suala hilo lisitekelezwe katika hali ambayo itawaumiza wengine hali inayofanya wafanyabiashara hao kujenga chuki na serikali,” Alisema Waziri Kitila Mkumbo.

Awali Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamachinga mkoa Kigoma (SHIUMA), Moran Mgina akizungumza mbele ya waziri Kitila Mkumbo alisema kuwa wafanyabiashara wameomba muda ili wahamishe bidhaa zao lakini Watendaji wa TAROADS wakitumia mgambo wa manispaa na polisi kutoka kituo kikuu cha polisi mkoa Kigoma wamekuwa wakitekeleza ubomoaji huo bila kutaka kusikiliza neno au ushauri wowote kutoka watu wengine.

Naye Mbunge wa jimbo la Kigoma Mjini, Revocatus Chipando (Baba Levo) alimweleza Waziri Mkumbo kwamba amepokea malalamiko makubwa ya wafanyabiashara kuhusu zoezi hilo na wapo wafanyabiashara waliotaka kulipa ili kubaki katika maeneo hayo lakini TANROADS wamekataa wakieleza watu hao waondoke na baadaye ndiyo maelekezo mengine ya nini wafanye au wapi waende  yatafuata.

Akijibu baadhi ya hoja zilizoibuliwa katika kongamano hilo Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa Kigoma, Mhandisi  Mwita Joram alisema kuwa wamefuata sheria na taratibu zote zinazotakiwa katika kutekeleza jambo hilo ikiwemo notisi iliyotolewa tangu mwaka jana lakini wengi hawakutekeleza.

Mwisho.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3