MAPATO YA MFUKO WA BARABARA TANZANIA YAONGEZEKA KWA ASILIMIA 45.
Kalimbaga ataja bandari na mizigo ya nchi jirani kuwa miongoni mwa vichocheo vya ukuaji wa mapato, atoa wito wa kuimarisha vyanzo endelevu vya ufadhili wa matengenezo ya barabara.
NAIROBI, KENYA.
Mapato ya Mfuko wa Barabara Tanzania yameongezeka kwa asilimia 45 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/20 hadi 2024/25, ongezeko lililochangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za bandari na usafirishaji wa mizigo ya nchi jirani kupitia Tanzania.
Takwimu hizo zimetolewa na Rais wa Umoja wa Mifuko ya Barabara Afrika (ARMFA), ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara Tanzania, Mhandisi Rashid S. Kalimbaga, akieleza umuhimu wa kutumia fursa zinazotokana na shughuli za kiuchumi na usafirishaji kuimarisha uwezo wa kugharamia matengenezo ya miundombinu ya barabara.
Kalimbaga ameyasema hayo jijini Nairobi, Kenya, Novemba 24, 2026, wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 23 wa ARMFA, unaowakutanisha wawakilishi wa nchi 35 na wadau mbalimbali wa sekta ya barabara na maendeleo.
Alisema ongezeko hilo linaonesha nafasi ya shughuli za bandari na usafirishaji wa mizigo inayopita Tanzania kwenda nchi jirani katika kuchochea ukuaji wa mapato ya Mfuko wa Barabara.
Kwa mujibu wa Kalimbaga, ameeleza umuhimu wa nchi za Afrika kuendelea kuimalisha kutafuta mifumo endelevu ya ufadhili wa matengenezo ya barabara, hasa ikizingatiwa kuwa miundombinu hiyo ni mhimili wa biashara na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi barani Afrika.
Akizungumzia mikakati ya kuimarisha mifumo hiyo katika bara la Afrika, Kalimbaga alitaja vipaumbele vitano vya uongozi wake wa miaka miwili katika ARMFA, ambavyo ni kuhakikisha upatikanaji wa fedha za uhakika, kuimarisha uhuru wa kiutendaji wa mifuko ya barabara, kujenga uwezo wa kitaasisi, kukuza ushirikiano na ubunifu pamoja na kuongeza ushawishi wa taasisi hiyo katika ngazi ya kikanda na kimataifa.
Alisema mifuko ya barabara inapaswa kuwa na uhuru wa usimamizi, rasilimali zinazotengwa kwa matumizi yaliyokusudiwa na mifumo madhubuti ya uwajibikaji ili kuhakikisha fedha zinazosimamiwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Aidha, alieleza umuhimu wa kupanua wigo wa vyanzo vya fedha kupitia ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, ufadhili wa tabianchi na mikataba inayozingatia matokeo, ili kupunguza utegemezi wa vyanzo vya kawaida vya mapato.
Kalimbaga alibainisha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya bidhaa zinazosafirishwa barani Afrika hutumia barabara, hivyo uwepo wa mifumo imara ya ufadhili wa matengenezo ni muhimu katika kuimarisha biashara, hususan kupitia Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), lenye soko la watu takribani bilioni 1.3.
Katika mkutano huo, amependekeza pia kuendelezwa kwa wazo la kuanzisha Mfuko wa Dhamana wa Bara la Afrika kwa ajili ya Matengenezo ya Barabara (FFC-ER), utakaolenga kuimarisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu hiyo.
Miongoni mwa maamuzi mengine yanayopendekezwa ni kupitishwa kwa dira mpya ya ARMFA na mpango kazi wenye gharama za utekelezaji pamoja na kuandaliwa kwa Mpango wa Kuboresha Utawala kwa kila Mfuko wa Barabara.
Mkutano huo wenye kaulimbiu isemayo “Mifuko ya Kizazi Kipya ya Matengenezo ya Barabara: Ufadhili wa Kiwango cha Bara, Muunganiko wa Kikanda na Ustahimilivu kwa Afrika Iliyounganishwa” unajadili mikakati ya kuimarisha mifumo ya ufadhili wa matengenezo ya barabara na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya kiuchumi barani Afrika.

.jpeg)
