Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
KIBOKO MAARUFU ZAIDI DUNIANI, FIONA, AFARIKI BAADA YA KUMEZA KOFIA ILIYOSOKOTWA KWA NYUZI

KIBOKO MAARUFU ZAIDI DUNIANI, FIONA, AFARIKI BAADA YA KUMEZA KOFIA ILIYOSOKOTWA KWA NYUZI

 

Fiona, kiboko ambaye alikuwa maarufu zaidi duniani tangu kuzaliwa kwake mwaka 2017, amefariki kwa huzuni katika Bustani ya Wanyama ya Cincinnati nchini Marekani baada ya kumeza kofia iliyosokotwa kwa nyuzi (knitted hat) ya mmoja wa wageni iliyokuwa imepeperushwa kwa bahati mbaya na upepo na kuingia kwenye eneo lake.

"Tunashiriki habari hizi za kusikitisha kwa huzuni kubwa. Fiona hakuweza kuokolewa licha ya juhudi kubwa za timu yetu ya madaktari wa mifugo na wahudumu wa wanyama," bustani hiyo ilisema katika taarifa yake siku ya Alhamisi.

Fiona alimeza kofia hiyo siku 10 kabla ya kufariki kwake, lakini mwanzoni hakukuwa na dalili zozote zilizoashiria kwamba angepata madhara makubwa kiasi hicho.

"Tumeshtuka sana kwa sasa. Hatukutarajia hili. Alipambana hadi dakika ya mwisho," alisema mkurugenzi wa bustani hiyo, Dave Jenaik.

Fiona alizaliwa Januari 2017 akiwa njiti sana, akiwa na uzito wa kilo 13 pekee, ambao ni takribani theluthi moja ya uzito wa kawaida wa mtoto wa kiboko.

Wahudumu wa bustani hiyo walianza kusimulia hatua kwa hatua maisha ya Fiona kupitia mitandao ya kijamii, wakionesha jinsi alivyopambana kuishi, kukua, kuogelea na kucheza. Jambo hilo lilimfanya kuwa maarufu duniani kote.

Umaarufu wake ulifikia hatua ya ladha ya aiskrimu kupewa jina lake, huku picha yake pia ikitumika katika onesho la ballet la The Nutcracker lililoandaliwa na kikundi cha sanaa cha eneo la Cincinnati.

Kifo chake pia kimekuja kabla ya wakati wake, kwani kwa mujibu wa wataalamu wa Bustani ya Wanyama ya Cincinnati, viboko wanaweza kuishi hadi miaka 50 wanapotunzwa kwenye mazingira ya kifungoni.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3