IKULU YA WHITE HOUSE YAMFUTA KAZI MKUU WA USALAMA WA MTANDAO BAADA YA HITILAFU KUBWA ZA MIFUMO
Mkuu wa usalama wa mtandao wa Marekani, Sean Cairncross, amefutwa kazi yake, chanzo kilicho karibu na Ikulu ya White House kimeiambia AFP siku ya Alhamisi, kufuatia hitilafu kubwa za mifumo na kuongezeka kwa wasiwasi kuhusu vitisho vinavyotokana na akili mnemba (AI).
Rais wa Marekani Donald Trump aliunga mkono kikamilifu uamuzi huo kwa madai kuwa Cairncross hakuwa na sifa stahiki za kutekeleza majukumu ya nafasi hiyo, chanzo hicho kimesema.
Majukumu yake yatatekelezwa kwa muda na Kirsten Davies, ambaye kwa sasa ni Afisa Mkuu wa Teknolojia ya Habari katika Wizara ya Ulinzi. Chanzo hicho kimesema Davies ana sifa zinazofaa zaidi kwa nafasi hiyo na tayari amethibitishwa na Seneti.
Katika siku na wiki za hivi karibuni, hitilafu kubwa za mifumo nchini Marekani zimeathiri usafiri, mawasiliano na biashara za mtandaoni kwa watumiaji wengi. Hitilafu hizo pia ziliathiri mtandao wa ndani wa mawasiliano wa siri za juu katika Shirika la Usalama wa Taifa (NSA).
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alimpongeza Davies kupitia mtandao wa X, akiandika: "Hongera kwa Mkurugenzi mpya wa Usalama wa Mtandao wa Taifa, Kirsten Davies. Natarajia kufanya kazi pamoja naye kuimarisha usalama wa mtandao wa Marekani."
Kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Mtandao wa Taifa, Cairncross alihudumu katika nyadhifa mbalimbali ndani ya Ikulu ya White House wakati wa muhula wa kwanza wa utawala wa Trump.

