IGP WAMBURA AIPA HEKO URA SACCOS.
MATUKIO DAIMA MEDIA
MOSHI
MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillus Wambura, amesema Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Usalama wa Raia (URA SACCOS) kimekuwa chombo muhimu cha kuboresha maisha ya kiuchumi na kijamii ya askari polisi na familia zao, kikichangia kujenga nyumba, kusomesha watoto na kuanzisha biashara.
Alisema mafanikio yaliyofikiwa na chama hicho katika kipindi cha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006, ni ushahidi kuwa mshikamano, nidhamu ya kifedha na utamaduni wa kuweka akiba vinaweza kubadilisha maisha ya watumishi na familia zao.
Wambura aliyasema hayo wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya URA SACCOS Limited yaliyofanyika jana katika viwanja vya Shule ya Polisi Tanzania (TPS), Moshi, mkoani Kilimanjaro.Alisema kupitia mikopo inayotolewa na chama hicho, wanachama wameweza kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo, ikiwamo kujenga na kuboresha makazi, kugharamia elimu ya watoto wao, kuanzisha na kukuza biashara pamoja na kununua mali.
"Mafanikio ya URA SACCOS hayaishii katika ukuaji wa mali na mtaji, bali yanaonekana pia katika familia zilizopata maendeleo, biashara zilizoanzishwa, ajira zilizotengenezwa na maisha yaliyobadilika," alisema Wambura.
Alisema ustawi wa askari ni sehemu muhimu ya utendaji wa Jeshi la Polisi, kwa kuwa mtumishi mwenye utulivu wa kiuchumi na kijamii anakuwa katika nafasi nzuri ya kutekeleza majukumu yake ya kulinda usalama wa wananchi.
Kwa mujibu wa IGP, katika kipindi cha miaka 20, URA SACCOS imepiga hatua kubwa, ikitoka kuwa na wanachama 4300 wakati wa kuanzishwa kwake hadi kufikia takribani wanachama 60,000.
.jpeg)

.jpeg)