Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 BONANZA LA TEF KUJENGA MSHIKAMANO WA WANAHABARI MORO...

BONANZA LA TEF KUJENGA MSHIKAMANO WA WANAHABARI MORO...


Matukio Daima Media, Morogoro.

Ushirikiano na mshikamano miongoni mwa wanahabari unatarajiwa kuimarishwa kupitia bonanza la michezo litakalowakutanisha wahariri wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na waandishi wa habari mkoani Morogoro, Novemba 27, 2026.

Bonanza hilo ni sehemu ya shughuli za Mkutano Mkuu wa Tisa wa TEF unaofanyika mkoani Morogoro, likiwa na lengo la kuwapa wahariri na waandishi wa habari nafasi ya kujenga mahusiano nje ya mazingira yao ya kawaida ya kazi, huku likihimiza umuhimu wa mazoezi ya mwili.

Michezo itakayoshindaniwa ni pamoja na soka, netiboli, kuvuta kamba, kukimbiza kuku, bao, kukimbia na magunia pamoja na riadha.

Msemaji na mratibu wa michezo wa TEF, Caren-Tausi Mbowe, amesema wahariri wamejiandaa kwa zaidi ya miezi miwili, huku baadhi ya washiriki wakishiriki michezo kulingana na umri na uwezo wao.

Naye msemaji wa timu ya waandishi wa habari Morogoro, Vincent Joseph, amesema kikosi chake kimejiandaa kwa zaidi ya mwezi mmoja na kipo tayari kukabiliana na timu ya TEF katika mchezo wa soka na michezo mingine.

Bonanza hilo limeungwa mkono mkono na wadau mbalimbali ambao wamechangia kufanikisha maandalizi yake, wakiwemo Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Mbunge wa Morogoro Mjini Abdulaziz Abood, Mbunge wa Viti Maalum Sheila Lukuba, baadhi ya madiwani wa Manispaa ya Morogoro na Hospitali ya Platinums.



Miongoni mwa wawakilishi wa wadau hao walioeleza ushiriki wao ni Ally Choholo, mwakilishi wa Mbunge Abdulaziz Abood, Mhagama Mhagama, mwakilishi wa Mbunge Sheila Lukuba; na Mussa Ruhamba kutoka Hospitali ya Platinums ambao wameeleza umuhimu wa Michezo katika kulinda afya miongoni mwa wanahabari na kujenga ushirikiano na mshikamano.

Platinum wakaahidi kutoa gari ya wagonjwa litakalokuwa Uwanjani wakati wote wa mchezo, watoa huduma ya kwanza na Fedha taslimu walizoahidi kukabidhi baadaye kusaidia gharama mbalimbali za maandalizi huku wakihusisha afya na umuhimu wa mazoezi.

Mwisho.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3