HUDUMA ZA JAMII KWENYE NYUMBA ZA IBADA HUWASOGEZA WANANCHI KARIBU
Nov 9, 2026
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WAUMIN wa dini ya kiislam mkoani Kigoma wametaka ujenzi wa misikiti na nyumba za ibada mkoani humo uzingatie uwepo wa huduma za kijamii ili kuzifanya nyumba hizo za ibada kuwa sehemu ya maisha ya wananchi wa mkoa huo.
Waumini hao walitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa Msikiti mkubwa wa ijumaa wa Mujahidina Ujiji manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo walisema kuwa uwepo wa huduma za kijamii ikiwemo za elimu naa afya zinafanya nyumba hizo kuwa karibu zaidi na wananchi wa kawaida.
Mmoja wa waumini hao, Athuman Luga alisema kuwa misikiti inayojengwa kwa ajili ya ibada pekee inakuwa siyo kimbilio la wananchi kwani watu ambao hawaendi kusali hawaisogeleo na wanaiona siyo sehemu ya maisha yao.
Naye Mussa Alli alisema kuwa nyumba za ibada zimekuwa zikijengwa kwa ajili ya kufanya ibada lakini uwepo wa huduma nyingine zikiwemo za elimu, afya kujenga ujuzi (ufundi) na masuala ya kibinadamu kunawafanya wananchi wote kusogea karibu na msikiti na huduma hizo na pia wakati mwingine inaongeza idadi ya waumini katika msikiti huo.
Akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa msikiti huo Imam Mkuu wa Msikiti Mujahidina na Muanzili wa ujenzi huo, Shekhe Hassan Kiburwa alisema kuwa uzinduzi wa mradi huo unalenga kujenga msikiti mkubwa wa ghorofa ambao utagharimu Zaidi ya shilingi Bilioni mbili.
Shekhe Kiburwa alisema kuwa pamoja na msikiti huo kuboreshwa kwa ajili ya ibada lakini pia kutakuwa na huduma nyingine muhimu za kijamii ikiwemo kituo cha masomo ya awali ya watoto (Chekechea), kituo cha ufundi mbalimbali ikiwemo ufundi cherehani, kituo cha kitoa huduma za afya na uwepo wa taasisi ambayo itasimamia changamoto za wanawake na watoto yatima.
Mwisho.





