ASKOFU MLAWI ATOA WITO WA MARIDHIANO, AAMINI AMANI NI MSINGI WA MAENDELEO YA TANZANIA
Nov 11, 2026
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Spiritual Pentecostal Church of Tanzania (SPCT) na Rais wa Tanzania Pastors Association (TPA), Dkt. Musa Samsoni Mlawi, amevitaka vyama vya siasa nchini vikiwemo CCM, Chadema na ACT Wazalendo kushiriki katika mazungumzo ya maridhiano yatakayosaidia kutatua tofauti zilizopo na kuimarisha umoja na mshikamano wa taifa.
Amesema hakuna changamoto inayoshindwa kutatuliwa kupitia mazungumzo yanayozingatia kuheshimiana, kusikilizana na kutanguliza maslahi ya taifa, hivyo ni muhimu kila upande kuwa tayari kukaa meza moja badala ya kuendeleza misimamo inayoweza kuongeza tofauti.
Awali, Askofu Mlawi alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuliongoza taifa na kutoa salamu kwa viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo pamoja na viongozi wa Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Novemba 11, 2026, Askofu Mlawi amesema maridhiano ni muhimu kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania na yanapaswa kuhusisha wadau mbalimbali ili kupata suluhu inayozingatia maoni ya pande zote.
Amesema amebaini baadhi ya vyama vya siasa vikiwa na msimamo wa kutokuwa tayari kushiriki katika meza ya maridhiano, hivyo amevitaka kutafakari upya msimamo huo na kukubali utaratibu utakaowezesha kila upande kusikilizwa.
" Mchakato huo haupaswi kuhusisha vyama vya siasa pekee, bali pia viongozi wa dini, mashirika ya haki za binadamu na wadau wengine wenye mchango katika kulinda haki na ustawi wa jamii, " Amesema Askofu Mlawi.
Akizungumzia nafasi ya taasisi za kidini, amesema katiba ya Tanzania Pastors Association inakitaka chama hicho kusimamia na kulinda amani, maelewano na kuheshimiana miongoni mwa Watanzania.
Amesisitiza kuwa haki na amani haviwezi kutenganishwa, hivyo kila upande unapaswa kuhakikisha haki za wananchi zinalindwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
Aidha, ameshauri katika mchakato huo kusikilizwa kwa viongozi waliowahi kulitumikia taifa kwa muda mrefu, akiwataja Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete na Mzee Wasira kuwa miongoni mwa viongozi ambao uzoefu wao unaweza kusaidia katika majadiliano.
Amesema washiriki wanapaswa kuweka kando mihemko, kujihesabia haki na kujipendelea, huku wakitambua kuwa katika mazungumzo kuna hoja zinazoweza kukubaliwa na nyingine kukataliwa.
Kuhusu amani, Askofu Mlawi amesema utulivu ni muhimu katika kulinda shughuli za kiuchumi, biashara na utalii, pamoja na kuendelea kuvutia wageni kutoka nje ya nchi.
Amewataka wananchi kuepuka vitendo vya vurugu na makundi ya ushawishi yanayoweza kuhatarisha amani, badala yake washiriki katika kudumisha utulivu, umoja na mshikamano.
Amesema kuna haja ya taifa kutafakari mwenendo wa maadili katika jamii, akitolea mfano tukio la binti aliyedhalilishwa kupitia mitandao ya kijamii, ambalo amesema limeleta taharuki na kusababisha madhara hata kwa wazazi wake.
Amesema utu wa binadamu unapaswa kuheshimiwa na kulindwa bila kujali jinsia, huku akisisitiza umuhimu wa jamii kukemea vitendo vya udhalilishaji vinavyofanyika katika mazingira mbalimbali, ikiwemo mitandao ya kijamii.
