WMA YATOA ELIMU YA VIPIMO KWA MAAFISA NA ASKARI WA JKT
Oct 2, 2026
Dodoma_
Wakala wa Vipimo (WMA) jana Oktoba 1, 2026 ilifanya ziara ya kutoa elimu ya matumizi sahihi ya vipimo kwa Maafisa na Askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika Makao Makuu ya Jeshi hilo yaliyopo eneo la Buigiri, Chamwino jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoa elimu hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka WMA, Bw. Francis Olwero, alisema amefurahishwa na mwitikio mkubwa na shauku waliyoionesha askari na maafisa wa JKT.
"Askari ni sehemu ya jamii, maisha yao kama yalivyo ya wananchi wengine yamezungukwa na vipimo kuanzia asubuhi hadi jioni. Ndio maana WMA iliona ni busara kuwaelimisha," alisema Olwero.
Alisema katika elimu hiyo, WMA imewasisitiza askari kuhoji na kujiridhisha kama vipimo vinavyotumika katika biashara mbalimbali wanazonunua vimehakikiwa na WMA, ikiwemo gesi ya kupikia, maji, umeme, mizani za madukani na sokoni na hata pampu za mafuta.
Kwa upande wake, Private Fatma Mohamed alisema elimu hiyo imemfungua macho kama mwananchi kujua haki yake.
"Mimi binafsi nimevutiwa na elimu hii, kama mwananchi nina haki ya kuhoji na kujiridhisha kama mizani ya buchani na hata pampu ya mafuta ya Sheli imehakikiwa na WMA kabla sijanunua bidhaa. Watanzania wenzangu hakikisheni mnafuatilia elimu inayotolewa na WMA ili kujua haki zenu kuhusu vipimo ili msipunjwe," alisema Private Fatma.
Naye Luteni Isaka Zacharia alisema ujio wa WMA umekuwa fursa muhimu kwa JKT.
"Tumejua kuwa tunapaswa kujiridhisha kuhusu matumizi ya vipimo sahihi kwenye huduma zinazogusa maisha yetu ya kila siku ikiwemo dira za maji na hata mita za umeme. Natoa rai kwa WMA kuendelea kutoa elimu ya vipimo kwa makundi mbalimbali katika jamii hususan wananchi wa kawaida na walioko vijijini," alisema Luteni Zacharia.
Private Michael Mdegela alisema elimu aliyoipata itamsaidia kuachana na mazoea ya kununua bidhaa bila kupima.
"Tumejifunza na tunaenda kuthibitisha hilo, maana kuanzia sasa tutaanza kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo na tutahoji kujiridhisha kama bidhaa tunazonunua zimepimwa kwa usahihi, hususan gesi ya kupikia. Kama gesi haijapimwa kwenye mzani uliohakikiwa na WMA, Siitaki!" alisisitiza.
Akifafanua kuhusu mkakati wa WMA, Meneja Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma kutoka WMA, Bi. Veronica Simba, amesema WMA inaendelea na zoezi la utoaji elimu ya vipimo kwa makundi mbalimbali katika jamii kwa kutumia mbinu mbalimbali za mawasiliano.
"Lengo letu ni kuhakikisha elimu ya matumizi sahihi ya vipimo inafika kwa kila mtu nchini, kwa kaulimbiu yetu isemayo, _Kipimo Sahihi ni Haki Yako_ alisema Bi. Simba.


