MAWAKALA WA UTALII KUTOKA INDIA WAVUTIWA NA HIFADHI ZA NGORONGORO NA SERENGETI
Oct 2, 2026
Mawakala wa utalii kutoka Jamhuri ya India wameelezea kuridhishwa na kuvutiwa na uzuri wa Hifadhi ya Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kufuatia ziara ya mafunzo (Fam Trip) iliyoandaliwa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kwa kushirikina na Ubalozi wa Tanzania Nchini India
Ziara hiyo yenye lengo la kuitangaza Tanzania katika soko la kimataifa la utalii, imewajumuisha mawakala 13 kutoka majiji mbalimbali ya India.
Wakizungumza mara baada ya ziara katika hifadhi ya Kreta ya Ngorongoro iliyotangazwa kama Ajabu ya Nane ya Dunia, walisema Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vya utalii vya kipekee duniani.
“Tumetembea nchi nyingi duniani, lakini kile tulichokiona hapa Ngorongoro ni cha tofauti sana. Muunganiko wa mandhari ya kuvutia, wingi wa wanyamapori katika eneo moja na uhifadhi uliotukuka ni jambo linaoonesha upekee wake, Hakika hii ni sehemu ambayo kila Mhindi anatakiwa kuja kuiona angalau mara moja maishani mwake,”
Kwa upande wa Serengeti, mawakala hao walipata fursa ya kushuhudia moja ya maajabu makubwa ya wanyamapori duniani, yakiwemo maelfu ya nyumbu na pundamilia katika harakati za uhamaji, pamoja na wanyama wakubwa watano (Big Five).
Mmoja wa mawakala hao alisema Serengeti imezidi matarajio yao.
“Tulikuwa tumesikia mengi kuhusu Serengeti kwenye filamu, lakini kuiona kwa macho yetu wenyewe ni hisia tofauti kabisa. Ni mbuga kubwa, ya asili na iliyohifadhiwa vizuri. Tuliona simba, chui na tembo kwa ukaribu. Huduma za malazi na ukarimu wa Watanzania ni wa hali ya juu,” alieleza.
Naye Afisa Masoko wa TTB Bwana Michael Ndaisaba alisema soko la India ni muhimu na linaendelea kukua kwa kasi, ambapo Ujio wa mawakala hao utachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya watalii kutoka Bara la Asia.
Ziara ya mawakala hao inatarajiwa kuhitimishwa jijini Zanzibar kwa kutembelea vivutio vya utalii wa fukwe na utamaduni.





