Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WAFANYABIASHARA KILOMBERO WATAKA HUDUMA ZA TRA ZISOGEZWE KARIBU

WAFANYABIASHARA KILOMBERO WATAKA HUDUMA ZA TRA ZISOGEZWE KARIBU

 

Kamishna Mkuu wa TRA CPA Yusuph Mwenda akizungumza na baadhi ya wafanyabiashara wa wilaya ya  Kilombero katika mji mdogo wa Ifakara

Matukio Daima Media, Morogoro 

Wafanyabiashara wilayani Kilombero, mkoani Morogoro, wameiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuongeza upatikanaji wa huduma za kikodi katika maeneo yao na kuendelea kutoa elimu ya mlipa kodi, wakieleza kuwa baadhi yao bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu wajibu na taratibu za ulipaji kodi.

Maombi hayo yametolewa na baadhi ya wafanyabiashara wa Mji Mdogo wa Ifakara wilayani Kilombero akiwemo Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao wilaya ya Kilombero Mohamed Msuya, wakati wa ziara ya Kamishna Mkuu wa TRA, CPA Yusuf Mwenda, wilayani humo, ambapo wafanyabiashara walieleza umuhimu wa kupata huduma zinazopatikana mijini bila kulazimika kukabiliana na changamoto za kuzifuata mbali na maeneo yao ya biashara

Wamesema elimu ya kodi ni muhimu katika kuwasaidia wafanyabiashara kuelewa matakwa ya sheria, kutekeleza wajibu wao kwa usahihi na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na kutofahamu taratibu za mamlaka hiyo.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa wilaya ya Kilombero, Mohammed Msuya, akichangia hoja katika kikao hicho

Changamoto hizo zinakuja wakati TRA ikiimarisha juhudi za kuongeza ushiriki wa walipa kodi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuifikisha Tanzania katika uchumi wa dola trilioni moja.

Akizungumza mkoani Morogoro katika shughuli tofauti za ziara yake, Mwenda amesema ushiriki wa sekta binafsi na walipa kodi ni muhimu katika kufanikisha malengo ya taifa, akibainisha kuwa utamaduni wa ulipaji kodi bado unahitaji kuimarishwa kupitia elimu zaidi.

Amegusia pia changamoto za baadhi ya walipa kodi, wakiwamo wakulima, katika kutumia mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFDs), pamoja na maombi ya kuboresha sheria za kodi ili kuendana na mahitaji ya walipa kodi bila kuathiri ukusanyaji wa mapato.


Katika ziara ya kiwanda cha Kilombero Sugar, Mkurugenzi wa Fedha wa kiwanda hicho, Fakii Fadhili, ameomba kuwepo kwa utaratibu maalumu wa kuwatambua walipa kodi wanaohusiana na kiwanda na wakulima, ili kurahisisha ulipaji kodi na kupunguza changamoto zinazowakabili.

Hoja hiyo inaangazia umuhimu wa kuzingatia mazingira ya shughuli za uzalishaji na uhusiano kati ya viwanda na wakulima katika kuboresha mifumo ya kodi.

Kwa upande mwingine, Mwenda amewataka watumishi wa TRA kufanya kazi kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya 2050 na kuimarisha ufanisi wa ukusanyaji mapato, huku akisisitiza kuwa walipa kodi hawapaswi kuonewa wala kunyimwa hakiza

Akifungua mafunzo ya ufuatiliaji na tathmini kwa wakuu wa idara wa TRA mjini Morogoro, amesema ushiriki wa sekta binafsi na utoaji wa elimu ya kodi ni miongoni mwa mambo muhimu katika kufanikisha malengo ya kiuchumi ya nchi.

Mafunzo hayo yanalenga kuimarisha utendaji wa watumishi, huku changamoto zilizotajwa zikijumuisha uhaba wa watumishi na wingi wa miradi inayotekelezwa na baadhi ya taasisi. Mafunzo hayo yanatarajiwa kuendelezwa kwa maafisa wa TRA wa ngazi za mikoa na wilaya.

TRA imeeleza msimamo wa kuhakikisha utekelezaji wa sheria za kodi unaenda sambamba na haki za walipa kodi, huku hatua za kisheria zikitarajiwa kuchukuliwa dhidi ya watumishi watakaobainika kuonea au kunyima haki walipa kodi.



Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3