TASHICO YAOMBA KUPANDISHA NAULI MV LIEMBA
Mkurugenzi udhibiti uchumi Shirika la Uwakala wa Meli (TASAC),Nahson Sigalla ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, akizungumza katika mkutano wa wadau wa usafiri na usafirishaji ziwa Tanganyika kupokea maoni ya kupandisha nauli ya meli ya Mv Liemba
Na Fadhili Abdallah, Kigoma
Mapendekezo yamewasilishwa kwa wadau wa usafiri na usafirishaji ziwa Tanganyika wakiombwa kutoa maoni yaliyowasilishwa kwao na Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) ikitoa mapendekezo ya kupandisha nauli za abiria na mizigo kwa meli ya MV Liemba inayotoa huduma za usafiri katika Ziwa Tanganyika, ikiwamo safari kutoka Kigoma kwenda Mpulungu nchini Zambia.
Afisa Uendeshaji wa TASHICO, Baraka Bigambo, akiwasilisha mapendekezo ya mabadiliko ya nauli kwa wadau wa usafiri wa majini mkoani Kigoma alisema kuwa kupanda kwa gharama za uendeshaji kumeifanya kampuni hiyo kuona umuhimu wa kupitia upya viwango vya sasa vya nauli za abiria na mizigo ili kukidhi mahitaji ya uendeshaji wa meli hiyo.
Sambamba na suala la kuomba mapendekezo ya kuongeza bei ya nauli pia shirika hilo limewasilisha pendekezo la kupunguza vituo vya kusimama kwa meli hiyo kutoka 18 vilivyopo sasa hadi kufikia tisa lengo ikiwa ni kupunguza muda wa meli hiyo kusafiri kutoka saa 48 inazotumia sasa hadi kufikia saa 24 kutoka bandari ya Kigoma hadi bandari ya Mpulungu nchini Zambia.
Meli hiyo ilisimama kutoa huduma mwaka 2018 na kuanza kufanyiwa matengenezo Julai 2024 kwa gharama ya shilingi bilioni 32 ambapo imeanza tena kutoa huduma
katika hali bora zaidi ikilinganishwa na ilivyokuwa kabla ya matengenezo, huku kurejea kwake katika huduma kukitarajiwa kuimarisha usafiri wa majini katika Ziwa Tanganyika.
Akifungua mkutano huo wa wadau Mkurugenzi udhibiti uchumi Shirika la Uwakala wa Meli (TASAC),Nahson Sigalla ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, alisema kuwa mkutano wa wadau umeandaliwa ili kupata maoni ya wananchi na wadau mbalimbali kuhusu mapendekezo ya viwango vipya vya nauli kabla ya Serikali kuridhia viwango vitakavyotumika.
Alisema wadau wamepewa fursa ya kuwasilisha maoni yao hadi Oktoba 30 mwaka huu, hatua inayolenga kuhakikisha maamuzi kuhusu mabadiliko ya nauli yanazingatia maoni ya wadau na hali halisi ya usafiri na usafirishaj majini ziwa Tanganyika.
Wakitoa maoni katika mkutano huo baadhi ya wasafirishaji Shehena katika ziwa Tanganyika akiwemo Mwenyekiti wa Wakala wa forodha ziwa Tanganyika, Dunia Shakuru ameitaka TASHICO kuangalia upya suala la nauli kwani inapingana na uhalisia kutokana na kuimarika kwa barabara hali ambayo italeta upinzani na kuifanya meli hiyo kukosa abiria wa kutosha.
Mdau mwingine aliyeshiriki katika mkutano huo, Zabron Balijue alisema kuwa kiwango cha gharama za kusafirisha mizigo kilichowekwa ni kikubwa ukilinganisha na matarajio ya wafanyabiashara wengi hali ambayo inaonesha meli hiyo imeingia kwenye biashara ya ushindani badala ya kutoa huduma hivyo akaomba viwango vya nauli za abiria na mizigo viangaliwe upya.
Mwisho.



