MKUMBO AMFARIJI MWENYEKITI WA KAMPUNI ZA UDALALI TANZANIA KWA KIFO CHA MKEWE
NA MATUKIO DAIMA MEDIA
MKURUGENZI wa Kampuni ya Udalali ya Kapondogoro Auction Mart, Methew Mkumbo, ameshiriki mazishi ya marehemu Stella Mosha, aliyekuwa mke wa Mwenyekiti wa Kampuni za Udalali Tanzania Fidelis katundu ,na kutoa salamu za pole kwa familia kufuatia msiba huo.
Mazishi hayo yaliyofanyika jana yalihudhuriwa na ndugu, jamaa, marafiki pamoja na wadau mbalimbali waliofika kuungana na familia katika kumpumzisha marehemu na kutoa faraja kwa wafiwa.
Akizungumza baada ya kushiriki mazishi hayo, Mkumbo alisema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Stella Mosha na kwamba ameguswa na msiba uliompata mwenyekiti huyo pamoja na familia yake.
Mkumbo alisema kipindi cha msiba ni wakati mgumu kwa familia, hivyo uwepo wa ndugu, jamaa, marafiki na wadau ni muhimu katika kuwapa moyo na kuwafariji wafiwa.
“Napenda kutoa pole nyingi kwa Mwenyekiti wetu, familia, ndugu, jamaa na marafiki wote kwa kuondokewa na mpendwa wao Stella Mosha Huu ni wakati mgumu sana kwa familia Tunawaombea Mungu awape nguvu, subira na faraja katika kipindi hiki cha majonzi,” alisema Mkumbo.
Aidha, Mkumbo alisema wadau wa sekta ya udalali wameguswa na msiba huo na wanaungana na mwenyekiti pamoja na familia yake katika kuomboleza.
Alisema kifo ni pigo kwa familia na jamii kwa ujumla, hivyo akawaomba wote walioguswa na msiba huo kuendelea kuwa karibu na familia na kuwapa moyo katika kipindi hiki.
Mkumbo alisema wataendelea kumuombea marehemu Stella Mosha apumzike kwa amani na familia yake iendelee kupata nguvu na faraja.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.

