WIZARA YA AFYA KUPELEKA HUDUMA ZA VIUNGO TIBA NA VIFAA SAIDIZI NGAZI ZOTE ZA AFYA
Na Lilian Kasenene, Morogoro
Matukio DaimaApp
WIZARA ya Afya imeahidi kuimarisha upatikanaji wa huduma za viungo tiba na vifaa saidizi katika vituo vya afya vya ngazi zote nchini, huku ikieleza kuwa huduma hizo pia zitaingizwa kwenye mfumo wa bima ya afya ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Hatua hiyo inalenga kuboresha huduma za matibabu na kuongeza ubora wa maisha kwa watu wanaohitaji huduma za urekebishaji wa viungo na vifaa saidizi..
Mkurugenzi wa tiba kutoka Wizara ya Afya Dk Hamady Nyembea alisema wizara imezingatia ujumuishaji wa huduma hii kwenye bima ya afya.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma za viungo tiba na vifaa saidizi mkoa wa Morogoro katika hospitali ya Mizinga Dk Nyembea alisema hatua hiyo ipo katika mpango mkakati wa miaka mitano wa wizara.
Alisema pamoja na kupeleka huduma hizi kwenye ngazi zote za huduma ya afya wizara pia inazingatia ubora wa huduma na vifaa saidizi vinavyotengenezwa kwa teknolojia za kisasa na vifaa vyepesi vinavyolingana na mahitaji halisi
"Ili kufikia malengo eneo hili pamoja na utafiti vinahitaji wataalam hivyo sekta binafsi ina nafasi kubwa kuongeza mchango wake ,"alisema Dk Nyembea
Alisema dhana ya huduma bora haiwezi kukamilika bila mgonjwa kupata uhalisi wa matibabu hivyo viungo tiba na vifaa saidizi ni nguzo muhimu katika mfumo wa afya.
"Huduma bora ni zile zinazojumuisha kukinga, kuzuia magonjwa, kutibu, kutengamaza na huduma shufaa,"alisema Dkt Nyembea.
Alisema watu wengi duniani wanaishi na ulemavu wa aina fulani na katika sensa ya mwaka 2022 inaonesha asilimia 11.2 wanaishi na ulemavu fulani hapa nchini.
Dk Nyembea alisema sababu kubwa zinazopelekea ulemavu ni pamoja na magonjwa yasiyoambukiza, ajali mbalimbali, matatizo ya kuzaliwa na kuongezeka kwa wazee.
Mwakilishi kutoka makao makuu ya Jeshi la Wananchi Tanzania Brigedia Jenerali Agatha Kafua aliomba wizara ya afya kushirikiana na hospitali ya Mzinga ili kutoa mafunzo kwa wataalamu wa vifaa tiba na saidizi.
Alisema ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi wanahitajika wataalamu na watumishi wa huduma ya viungo tiba na vifaa saidizi wa kutosha.



