Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
UN YAITAKA TANZANIA KUSITISHA UHAMISHAJI WA WAMASAI NGORONGORO NA LOLIONDO

UN YAITAKA TANZANIA KUSITISHA UHAMISHAJI WA WAMASAI NGORONGORO NA LOLIONDO

 


Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Kutokomeza Ubaguzi wa Rangi (CERD) imeitaka Tanzania kusitisha mara moja kile ilichokitaja kuwa uhamishaji wa nguvu wa jamii ya Wamasai kutoka makazi ya mababu zao katika Ngorongoro na Loliondo.

Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa, Agosti 28, kamati hiyo ilieleza wasiwasi kuhusu madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya jamii hiyo, ikiwemo kufukuzwa na kuhamishwa kwa nguvu, pamoja na vikwazo vya kupata ardhi za mababu, maeneo ya makazi na rasilimali za asili.

CERD pia iliitaka serikali ya Tanzania kuchunguza na kushughulikia madai ya ukiukwaji wa sheria yaliyoripotiwa, yakiwemo kukamatwa holela kwa baadhi ya wakazi na matumizi ya nguvu kupita kiasi na vyombo vya dola.

Kamati hiyo ilisema Tanzania inapaswa kurejesha na kuboresha upatikanaji wa huduma za msingi katika maeneo husika, zikiwemo elimu, huduma za afya, maji safi na huduma za usafi wa mazingira.

Aidha, ilitoa wito kwa mamlaka za Tanzania kuhakikisha mazingira salama kwa watetezi wa haki za binadamu, mashirika ya kiraia, wanaharakati, wanasheria na waandishi wa habari wanaoshughulikia masuala yanayohusu haki za jamii za wenyeji.

Katika mapendekezo yake, CERD iliitaka Tanzania kutangaza haraka matokeo na mapendekezo ya tume mbili za rais zilizoundwa Februari 2025 kuchunguza sera za matumizi ya ardhi, uhamishaji wa wakazi na uhifadhi ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Kamati hiyo pia ilisisitiza umuhimu wa kuhakikisha jamii ya Wamasai inashirikishwa kikamilifu katika maamuzi yanayohusu mustakabali wa maeneo wanayoishi na kuyategemea kwa maisha yao.

Serikali ya Tanzania mara kadhaa imekuwa ikisisitiza kuhusu matumizi ya maeneo hayo kwa manufaa ya umma, ikizingatia sheria na masuala ya haki za binadamu.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3