Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
TUME YA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI  YAANZA UKAGUZI KWA WAKUSANYAJI NA WACHAKATAJI WA TAARIFA HIZO  NCHINI.

TUME YA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI YAANZA UKAGUZI KWA WAKUSANYAJI NA WACHAKATAJI WA TAARIFA HIZO NCHINI.

 Na Mwandishi Wetu.

Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imeanza zoezi la ukaguzi wa uzingatiaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44, kwa kutembelea taasisi, mashirika na wafanyabiashara wanaokusanya na kuchakata taarifa binafsi nchini.

Hayo yameelezwa leo, Agosti 28, 2026 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dkt. Emmanuel Mkilia wakati akizungumza na vyombo vya habari ambapo amesema ukaguzi huo wa kutembelea taasisi, mashirika na wafanyabiashara mbalimbali nchini unalenga kujiridhisha iwapo wakusanyaji na wachakataji wa taarifa binafsi wanazingatia matakwa ya sheria katika shughuli zao.

Miongoni mwa mambo yatakayokaguliwa ni usajili wa taasisi katika rejesta ya Tume, utekelezaji wa majukumu ya Afisa Ulinzi wa Taarifa (DPO) katika taasisi husika, pamoja na namna taarifa binafsi zinavyokusanywa, kuchakatwa na kuhifadhiwa ili kuhakikisha taratibu zilizowekwa kisheria zinafuatwa.

Eneo jingine litakalokaguliwa ni utaratibu unaotumika kusafirisha taarifa binafsi nje ya nchi, kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa chini ya Vifungu vya 31 na 32 vya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

Aidha, PDPC imeeleza kuwa itachunguza hatua zinazochukuliwa na taasisi katika kulinda taarifa binafsi dhidi ya upotevu, uteketezaji, ubadilishaji au kuchakatwa bila idhini, kama inavyoelekezwa katika Kifungu cha 27(1) cha sheria hiyo.

Ukaguzi huo ni moja ya majukumu ya Tume na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya taasisi, mashirika au wafanyabiashara watakaobainika kutokidhi matakwa ya sheria, ikiwamo kutolewa kwa adhabu na faini kwa mujibu wa sheria.












Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3