Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
TTCL YALENGA KAYA ZAIDI 400,000 KATIKA AWAMU MPYA YA FAIBA MLANGONI KWAKO

TTCL YALENGA KAYA ZAIDI 400,000 KATIKA AWAMU MPYA YA FAIBA MLANGONI KWAKO

 

Na Matukio DaimaMedia 


Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeanza utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Faiba Mlangoni Kwako (Fiber to the Home–FTTH), likilenga kuongeza zaidi ya Home Pass 400,000 ili kupanua upatikanaji wa intaneti yenye kasi kwa wananchi, taasisi na wafanyabiashara nchini.


Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa awamu hiyo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amesema Serikali inataka huduma hiyo ifike katika maeneo yenye makazi yanayokua, masoko, maeneo ya biashara, viwanda, shule, vyuo, vituo vya afya na ofisi za Serikali Tanzania Bara na Zanzibar.

Amesema mafanikio ya mradi huo hayataangaliwa kwa idadi ya miundombinu itakayojengwa pekee, bali pia kwa wananchi watakaounganishwa, ubora na kasi ya intaneti pamoja na kiwango cha kuridhika kwa wateja.

“Mradi wa Faiba Mlangoni Kwako si ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano pekee, bali ni hatua ya kimkakati ya kufungua fursa za elimu, biashara, ajira na ubunifu, na kuchochea ujenzi wa uchumi wa kidijitali nchini,” amesema.

Waziri Kairuki ameitaka TTCL kuhakikisha huduma hiyo inatolewa kwa ubora, uhakika na gharama zinazomudu wananchi, huku ikiboresha mifumo ya huduma kwa wateja, hasa katika kushughulikia malalamiko kwa wakati na kwa ufanisi.


Aidha, ameagiza shirika hilo kuandaa vifurushi vinavyokidhi mahitaji na uwezo wa makundi mbalimbali, yakiwemo familia, wanafunzi, vijana na wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, utekelezaji wa mradi huo pia unatakiwa kusimamiwa kwa kuzingatia uwajibikaji na nidhamu ya kibiashara, huku wazabuni na wakandarasi wakihakikisha kazi zinakamilika kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kwa kuzingatia thamani ya fedha inayowekezwa.


Amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali wa mwaka 2024–2034, unaolenga kuongeza matumizi ya teknolojia na upatikanaji wa huduma za Serikali kwa njia za kidijitali.

Ameeleza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kuhakikisha ifikapo mwaka huo angalau asilimia 70 ya wananchi wanatumia TEHAMA, huku zaidi ya asilimia 80 ya huduma za Serikali zikitolewa kwa njia ya kidijitali iliyo salama na jumuishi.

Akizungumzia hali ya matumizi ya intaneti nchini, Waziri Kairuki ametumia takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa robo mwaka iliyoishia Juni 2026, akisema usajili wa intaneti ulifikia 62,793,986, wakati matumizi ya data yalifikia Petabaiti 1,041.


Hata hivyo, amesema idadi ya usajili wa huduma ya Faiba Nyumbani ilikuwa 178,904, jambo linaloonyesha kuwa bado kuna nafasi kubwa ya kuongeza matumizi ya intaneti ya kasi kupitia teknolojia ya nyuzi za macho.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, amesema kuanza kwa Awamu ya Pili ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Biashara wa Miaka 10 wa shirika hilo kwa kipindi cha 2025/26 hadi 2034/35.



Marwa amesema TTCL imefikia hatua hiyo ikiwa tayari imejenga msingi kupitia Awamu ya Kwanza ya mradi huo, ambapo shirika limefanikiwa kujenga zaidi ya Home Pass 280,000 na kufikisha jumla ya maungio ya huduma ya nyuzi za macho karibu 300,000 nchini.



Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3