Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 SERIKALI KUTUMIA SH1.39 TRILIONI KUKARABATI VIFAA TIBA

SERIKALI KUTUMIA SH1.39 TRILIONI KUKARABATI VIFAA TIBA

Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media DODOMA.

 SERIKALI inatarajia kutumia Sh1.39 trilioni hadi mwaka 2036 katika matengenezo ya vifaa tiba nchini, hatua inayolenga kuhakikisha mashine zinazotumika hospitalini zinaendelea kufanya kazi na wananchi kupata huduma za afya kwa wakati.

Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Eliudi Eliakimu, amesema fedha hizo zitatumika katika kuimarisha matengenezo ya vifaa tiba, huku akibainisha kuwa Serikali inakadiriwa kutumia wastani wa Sh139.5 bilioni kwa mwaka katika eneo hilo.

Dk. Eliakimu amesema hayo Alhamisi, Agosti 27, 2026, jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa Usimamizi wa Vifaa Tiba pamoja na mafunzo kwa wahandisi na watumiaji wa vifaa hivyo.

Amesema pamoja na Serikali kuendelea kununua na kusambaza vifaa tiba katika vituo vya afya na hospitali za ngazi mbalimbali, baadhi ya vifaa vimekuwa vikisimama kufanya kazi vinapoharibika kutokana na ukosefu wa fedha za matengenezo.

Kutokana na hali hiyo, amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa hospitali kutenga asilimia 10 ya mapato ya hospitali kwa ajili ya matengenezo ya vifaa tiba.

“Ni aibu kwa hospitali kuwa na vifaa tiba vya kisasa lakini havifanyi kazi kutokana na kukosa fedha za matengenezo.

Ninawaagiza leo RMO, DMO na Wakurugenzi Watendaji kuhakikisha

 mnatenga asilimia 10 ya mapato yenu na kuielekeza kwenye matengenezo ya vifaa tiba ili wananchi wasikose huduma,” amesema Dk. Eliakimu.

Aidha, amesema hospitali zinapaswa kutenga asilimia moja ya mapato yake kwa ajili ya kujenga uwezo wa wahandisi na mafundi wa vifaa tiba, ili waweze kufanya matengenezo ya vifaa vinapoharibika.

Mshauri Mwelekezi kutoka Wizara ya Afya, Gerald Mrema, amesema Mwongozo wa Usimamizi wa Vifaa Tiba utasaidia kuweka utaratibu wa kuhakikisha vifaa vilivyonunuliwa vinaendelea kutumika badala ya kuachwa vinapoharibika.

Amesema utekelezaji wa mwongozo huo utasaidia kupunguza malalamiko ya wananchi wanaokosa huduma kutokana na mashine kuharibika, kwa kuwa hospitali zitakuwa na mipango na bajeti maalumu za matengenezo.

“Kwenye hospitali zetu kuna vifaa vingi ambavyo havifanyi kazi wengine hawana hata ofisi za watumishi kufanyia kazi, lakini kuna vyumba maalumu vya kuhifadhi mashine mbovu baada ya mwongozo huu hatutarajii kukuta mashine haifanyi kazi kutokana na ubovu,” amesema Mrema.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Vifaa Tiba kutoka Taasisi ya Ifakara Health Institute, Hope Peter, amesema taasisi hiyo inaunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha usimamizi na matengenezo ya vifaa tiba nchini.

Amesema kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, wamekuwa wakitoa mafunzo ya matengenezo ya vifaa tiba kwa wahandisi na mafundi kutoka vituo 25 vya kutolea huduma za afya.

“Mwongozo huu utasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha utendaji kazi wa wahandisi wa vifaa tiba na hospitali kwa ujumla, kuhakikisha vifaa vinakuwa katika hali nzuri na huduma zinapatikana pale zinapohitajika,” amesema Peter.

Hata hivyo, amesema sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa wahandisi na mafundi wa vifaa tiba, mazingira duni ya kufanyia kazi pamoja na uhaba wa vipuri.

Amesema vifaa vingi vya tiba hununuliwa kutoka nje ya nchi na vinapoharibika, upatikanaji wa vipuri huwa changamoto, hali inayosababisha baadhi ya mashine kukaa muda mrefu bila kufanya kazi.

Peter ameshauri Serikali kuongeza idadi ya wataalamu wa vifaa tiba, kutenga bajeti maalumu ya matengenezo na ununuzi wa vipuri, pamoja na kuboresha mazingira ya kazi kwa kujenga karakana na maeneo salama ya kuhifadhi na kufanyia matengenezo vifaa hivyo.

Amesema hatua hizo zitasaidia kuongeza muda wa matumizi ya vifaa tiba, kuboresha ufanisi wake na kuhakikisha wananchi wanapata huduma wanazohitaji kwa wakati.

Mwisho

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3