MWAMUZI OMAR ABDULKADIR ARTAN, KUCHEZESHA FAINALI YA CECAFA KAGAME CUP 2026
Mwamuzi bora wa Afrika wa mwaka 2025, Omar Abdulkadir Artan wa Somalia, ameteuliwa kuchezesha Fainali ya Kombe la CECAFA Kagame 2026.
Artan atasaidiwa na Waamuzi wasaidizi Liban Abdulrazack wa Djibouti na Eliezer Stephen Yiembe wa Kenya. Watatu hao pia wameteuliwa kusimamia mechi ya UEFA Super Cup itakayofanyika Agosti 12 mjini Salzburg.
Fainali ya Kombe la CECAFA Kagame itachezwa Agosti 7 katika Uwanja wa Amahoro, Kigali, Rwanda.
Artan ameendelea kujijengea sifa kama mmoja wa Waamuzi bora barani Afrika, huku mafanikio yake yakihamasisha kizazi kipya cha Waamuzi kote barani.
Waamuzi hao wanatarajiwa kuwasili Kigali Jumanne kwa ajili ya maandalizi ya fainali ya CECAFA Kagame, ambayo pia itatumika kama sehemu ya maandalizi yao kuelekea mechi ya UEFA Super Cup ya mwaka 2026 kati ya mabingwa wa UEFA Champions League, Paris Saint-Germain, na mabingwa wa UEFA Europa League, Aston Villa FC.
Mechi za nusu fainali za Kombe la CECAFA Kagame zitachezwa Agosti 4, ambapo Gor Mahia FC ya Kenya itakutana na Al Hilal SC, huku wenyeji Rayon Sports FC wakivaana na Jamus SC ya Sudan Kusini.
Bingwa wa mashindano hayo atajinyakulia kitita cha Dola za Marekani 30,000, mshindi wa pili atapata Dola 20,000, huku mshindi wa tatu akiondoka na Dola 10,000.
