Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MPANGA-KIPENGERE YANG’ARA AFRIKA, YASHINDA TUZO YA UTALII YA DUNIA 2026

MPANGA-KIPENGERE YANG’ARA AFRIKA, YASHINDA TUZO YA UTALII YA DUNIA 2026


Na Samwel Mpogole – Mbeya


Tanzania imeendelea kuandika historia katika sekta ya utalii baada ya Hifadhi ya Mpanga-Kipengere, inayosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), kutwaa tuzo ya kimataifa ya Africa’s Leading Honeymoon Destination 2026 katika mashindano ya World Travel Awards 2026.


Ushindi huo umetangazwa katika hafla iliyofanyika Bwejuu, Zanzibar, huku ikiwa ni mara ya kwanza kwa TAWA kushiriki katika mashindano hayo makubwa ya kimataifa yanayotambua ubora na umahiri katika sekta ya utalii duniani.


Mpanga-Kipengere imeibuka mshindi baada ya kushindanishwa na maeneo mbalimbali ya utalii kutoka mataifa ya Afrika, yakiwemo Misri, Afrika Kusini, Botswana, Rwanda na Morocco, na hatimaye Tanzania kuibuka kidedea kupitia kivutio hicho kinachozidi kupata umaarufu katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.



Akizungumza baada ya ushindi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Meja Jenerali Mstaafu Hamis Semfuko, amesema mafanikio hayo yametokana na ubunifu, bidii na ushirikiano wa karibu kati ya Bodi, Menejimenti na watumishi wa TAWA, pamoja na Watanzania walioshiriki katika zoezi la kupiga kura.


Amesema ushindi huo ni chachu ya kuendelea kuimarisha utalii wa ndani na kuongeza nguvu katika kuitangaza Tanzania kuwa miongoni mwa maeneo bora ya utalii duniani.


Mpanga-Kipengere, iliyopo katika mikoa ya Mbeya na Njombe, ni miongoni mwa maeneo yenye vivutio vya kipekee katika Nyanda za Juu Kusini, ikiwemo maporomoko ya maji, mandhari ya kuvutia, ndege wa aina mbalimbali na uoto wa asili unaovutia watalii.



Mbali na uzuri wa asili, eneo hilo pia lina historia muhimu inayohusishwa na Chifu Mkwawa, jambo linaloongeza thamani ya eneo hilo katika nyanja za utalii wa ikolojia, historia na utamaduni.


Wadau wa utalii wanaeleza kuwa ushindi huo unaweza kuwa fursa kubwa ya kuitangaza zaidi Mpanga-Kipengere ndani na nje ya Tanzania, kuongeza idadi ya watalii, kukuza biashara zinazohusiana na utalii na kutoa fursa zaidi za kiuchumi kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka hifadhi hiyo.


Kwa ushindi huo, Mpanga-Kipengere imeendelea kuthibitisha kuwa Nyanda za Juu Kusini siyo tu kitovu cha kilimo na maliasili, bali pia ni eneo lenye fursa kubwa katika utalii wa kimataifa.


Ushindi wa Africa’s Leading Honeymoon Destination 2026 hivyo unaweka Mpanga-Kipengere katika ramani ya maeneo yanayoweza kuwa chaguo bora kwa watalii wanaotafuta utulivu, mandhari ya asili na uzoefu wa kipekee wa utalii wa kimapenzi barani Afrika.




Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3