MAONESHO YA YST YAIBUA HAMASA YA SAYANSI KWA WANAFUNZI LINDI
Na Hadija omary
Maonesho ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania YST yameelezwa kuwa ni chachu na hamasa kwa Mkoa wa Lindi katika kuongeza ushiriki wa wanafunzi wa shule za sekondari katika masomo ya sayansi na kujifunza kupitia majaribio.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Bi. Victoria Mwanziva wakati wa maonesho ya kazi bunifu za sayansi na teknolojia yaliyofanyika huko Manispaa ya Lindi.
Mwanziva amesema maonesho hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuibua vipaji na kuwavutia wanafunzi wengi kupenda na kufaulu masomo ya sayansi.
Kwa upande wake Mwanzilishi mwenza wa Shirikisho la Wanasayansi Chipukizi Tanzania YST, Dkt. Gozibert Kamugisha, amesema huu ni msimu wa tano kwa Mkoa wa Lindi kushiriki maonesho hayo na yamekuwa na manufaa makubwa kwa wanafunzi katika kubuni na kutatua matatizo ya jamii kupitia sayansi.
Amesema YST ni jukwaa ambalo linajitahidi kujenga utamaduni kwa vijana kwa kufanya utafiti na kugundua vitu vipya kiasi kwamba Hata wanavyoendelea kukua na kuendelea na masomo Yao utafiti uwe ni swala la kiutamaduni na lisiwe swala la kuelekezwa." alieleza Kamugisha
Ameongeza kuwa lengo la kuyafanyia hayo yote ni kutengeneza kizazi ambacho kinaweza kuchukua jukumu la moja kwa moja kumaliza matatizo yanayowakabili Watu kuliko kusubiri Serikali ama wafadhiri kwa ajili ya kutatua matatizo hayo.
Aidha Mshauri wa Masuala ya Kijamii kutoka Kampuni ya Shell ambao ni wadhamini wa maonesho hayo, Bi. Msomis Mbena, amesema kupitia program hiyo wanafunzi wamewezeshwa kufanya bunifu mbalimbali zitakazosaidia kutatua changamoto za kila siku.
"Program hii ya YST inaendana na mikakati wetu wa kimataifa wa kundeleza elimu ya Sem huku ikichangia maendeleo ya ujuzi kwa kuwasaidia wanafunzi kukuza uwezo wa kufanya utafiti, ugunduzi pamoja na kutafuta changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii" alisema Mbena
Kwa upande wake Afisa Elimu Sekondari Manispaa ya Lindi Mwalimu Rehema Nahale ametumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa YST kwa msaada wao wa kuwasaidia wanafunzi kufanya uvumbuzi wa matatizo mbalimbali yanayotokea katika jamii .
" Hakika nafasi hii ni kubwa Sana kwao na wataichukua elimu hii sio tu kwa kujifunza kwa ubinafsi wao bali watasaidia matatizo ya jamii kwa ujumla lakini hii itakuwa faida kwao kwa elimu ya kivitindo itakuwa imebaki vichwani mwao " alisema Nahale
Katika maonesho hayo shule tatu zilizoshinda zimepata nafasi ya kuwakilisha Mkoa wa Lindi katika mashindano ya kitaifa yatakayofanyika Jijini Dar es Salaam.






