KENYA YATUMA OMBI LA KUANDAA MASHINDANO YA DUNIA YA RIADHA 2029
Jiji kuu la Kenya, Nairobi, imewasilisha rasmi ombi la kuandaa Mashindano ya Dunia ya Riadha mwaka 2029, ikiwa na lengo la kuwa mji wa kwanza barani Afrika kuandaa mashindano hayo makubwa ya riadha.
Mji mkuu wa Kenya unashindana na London, Rome na Munich kuwania haki ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.
Serikali ya Kenya imetoa dhamana ya kuunga mkono zabuni hiyo kikamilifu, ikiwemo kuboresha miundombinu, usalama na maandalizi ya kiutawala yanayohitajika kuandaa mashindano hayo.
Kenya tayari ina uzoefu wa kuandaa mashindano makubwa ya riadha.
Mombasa iliandaa Mashindano ya Dunia ya Mbio za Nyika mwaka 2007, huku Nairobi ikiwa mwenyeji wa Mashindano ya Dunia ya Riadha kwa Wanariadha walio chini ya miaka 18 mwaka 2017 na yale ya chini ya miaka 20 mwaka 2021.
Nairobi pia iliandaa Mashindano ya Riadha ya Afrika mwaka 2010.
Shirikisho la Dunia la Riadha, World Athletics, linatarajiwa kutangaza mji utakaokuwa mwenyeji wa mashindano ya mwaka 2029 mwezi Septemba.