INFANTINO AOMBA RADHI,BADO NI RAIS WA FIFA
Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) Gianni Infantino, ameomba radhi kwa makosa yaliyofanyika katika mpango uliokuwa ukilenga kuuza sehemu ya hisa za mashindano ya FIFA kwa wawekezaji binafsi kupitia kampuni tanzu ya FIFA Forward Enterprise (FFE). Licha ya kukosolewa vikali, viongozi wakuu wa FIFA wameendelea kumuunga mkono na kuthibitisha kuwa ataendelea kushika nafasi yake kama Rais wa shirikisho hilo.
Infantino, ambaye alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Rais wa FIFA mwaka 2016 baada ya kuondoka kwa mtangulizi wake Sepp Blatter kufuatia kashfa za ufisadi, amekuwa akiongoza shirikisho hilo kwa takriban muongo mmoja. Kwa sasa anajiandaa kuwania muhula wa 4 katika uchaguzi wa urais wa FIFA unaotarajiwa kufanyika Machi 2027.
Sakata hilo lilizuka baada ya kubainika kuwa Infantino alikuwa amependekeza kuanzishwa kwa kampuni ya FFE ambayo ingeruhusu wawekezaji binafsi kununua hisa katika haki za kibiashara na tiketi za mashindano makubwa ya FIFA, ikiwemo Kombe la Dunia la Wanaume na Wanawake. Mpango huo ulipingwa vikali na UEFA pamoja na baadhi ya viongozi wa ndani ya FIFA kwa madai kuwa uliandaliwa kwa siri, haukuwa na uwazi wa kutosha na ungeweza kuhatarisha uhuru wa usimamizi wa mashindano hayo.
Katika kikao cha dharura kilichofanyika Rabat, Morocco, Infantino na Katibu Mkuu wa FIFA, Mattias Grafstrom, walikiri kuwa kulikuwa na dosari katika namna mpango huo ulivyoandaliwa na kuwasilishwa bila ushirikishwaji wa kutosha wa wadau.
Wawili hao pia waliwatumia viongozi wa Vyama wanachama barua ya kuomba radhi na kuahidi makosa kama hayo hayatatokea tena, huku FIFA ikisisitiza kuwa taratibu zake za utawala hazikuvunjwa.
Hata hivyo, shinikizo dhidi ya Infantino bado linaendelea, huku UEFA ikitangaza kupoteza imani na uongozi wake na baadhi ya vyama vya soka barani Ulaya vikiacha kuunga mkono nia yake ya kugombea muhula wa nne mwaka 2027.
Pamoja na hali hiyo, Infantino bado anaungwa mkono na mataifa kadhaa, hasa kutoka Afrika na Asia, jambo linalompa nafasi kubwa ya kuendelea kuongoza FIFA.