Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 GIZ YAAHIDI KUTOA EURO MILIONI 39.8 KWA AJILI YA KUIMARISHA BIASHARA YA KIKANDA.

GIZ YAAHIDI KUTOA EURO MILIONI 39.8 KWA AJILI YA KUIMARISHA BIASHARA YA KIKANDA.


Na,Jusline Marco;Arusha

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jamhuri ya Shirikisho ya Ujerumani zimethibitisha upya nia yao ya kuendeleza ushirikiano wa kikanda kufuatia kuhitimishwa kwa majadiliano ya 

Ushirikiano wa Maendeleo, huku Ujerumani ikiahidi kutoa ruzuku mpya ya Euro milioni 39.8 kwa ajili ya kuimarisha biashara ya kikanda na ushirikiano wa kiuchumi katika eneo hilo.

Akizungumza wakati wa mkutano wa pande mbili na ujumbe huo wa kusaini makubaliano ya fedha hizo, Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Balozi Stephen P.  Mbundi ameushukuru uongozi wa Jamhuri ya Shirikisho ya Ujerumani kwa kuwa mshirika wa muda mrefu wa EAC, huku akibainisha kuwa ushirikiano endelevu wa nchi hiyo umechangia kwa kiasi kikubwa katika safari ya Jumuiya hiyo ya ushirikiano wa kikanda.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayeshughulikia Masuala ya Forodha, Biashara na Fedha, Bi. Annette Ssemuwemba, mbali na kuushukuru ujumbe huo kwa dhamira yao ya kuiunga mkono Jumuiya hiyo, alibainisha kuwa mazungumzo hayo yalifanyika wakati mwafaka ambapo EAC inaanzisha utekelezaji wa Mkakati wake wa 7 wa Maendeleo.

" Tunaishukuru Ujerumani kwa kukaa nasi mezani ili kupitia upya vipaumbele vyetu na kubainisha maeneo ambayo tunaweza kushirikiana ili kupata matokeo, hii ndiyo roho ya ushirikiano na uwajibikaji wa pamoja ambayo ni muhimu katika kufikia malengo ya ajenda yetu ya ushirikiano wa kikanda," alisema Bi. Ssemuwemba.

Mazungumzo hayo yalilenga katika kuunga mkono Mkakati wa 7 wa Maendeleo wa EAC, wakati wa majadiliano hayo, Ujerumani na EAC zilikubaliana kuwa jukumu kuu ni kuendeleza zaidi Biashara ya Afrika Mashariki na ushirikiano wa kiuchumi wa kanda hiyo ambapo Ujerumani imeahidi kutoa ruzuku ya euro milioni 39.8 kwa ajili ya lengo hili.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Afrika Mashariki na Kati katika Wizara ya Shirikisho ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (BMZ), Joachim Schmitt, akizungumza alisema kuwa "Afrika Mashariki ndiyo kanda inayokua kwa kasi zaidi, ikishuhudia ongezeko la asilimia 14 katika biashara ya ndani ya EAC, pamoja na kukua kwa kiasi cha biashara ndani ya AfCFTA na nje ya bara hilo, amesema kanda hiyo ni kitovu cha kuvutia  uwekezaji kwa sekta binafsi ya Ujerumani na Ulaya inayopenda kujihusisha na biashara na uendelezaji wa mnyororo wa thamani.

Aliongeza kuwa kupitia ushirikiano huo wamelenga kuunga mkono ushirikiano wa kibiashara unaozingatia kanuni na sheria, maendeleo ya kiuchumi ya kikanda, pamoja na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi ambapo fedha zilizotengwa zitalenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa biashara ndogo ndogo na za kati katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kupitia ushirikiano kati ya benki ya maendeleo ya Ujerumani na Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki huku sehemu ya fedha hizo zitaboresha upatikanaji wa fedha kwa biashara hizo kupitia ushirikiano kati ya  Benki hizo.

Sambamba na hayo washirika wote wawili walisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu na uratibu na asasi za kiraia, sekta binafsi na washirika wa maendeleo ili kuimarisha ushirikiano wa kikanda ambapo Ujerumani itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Umoja wa Ulaya pamoja na nchi zote wanachama zinazoshiriki, ili kusaidia mipango ya kikanda katika nyanja za biashara, mabadiliko ya kidijitali, afya, usimamizi wa maji ya mipakani, asasi za kiraia na maendeleo endelevu ya kiuchumi.

Aliongeza kuwa katika mgao wa fedha hizo,  kiasi cha Euro milioni 4.8 kimetengwa kama msaada wa ziada ili kukabiliana na mlipuko wa Ebola unaoendelea ambapo fedha hizi zitaelekezwa kwenye hatua za moja kwa moja za kujiandaa, kuzuia na kukabiliana na Ebola, pamoja na kuimarisha kwa ujumla uwezo na uratibu wa kikanda, shughuli hizo ambazo zitatekelezwa kupitia mradi wa EAC/GIZ unaoitwa "Support to Pandemic Preparedness in the EAC Region" (PanPrep), ambao umekuwa ukilisaidia eneo hilo tangu mwaka 2017.

Rasilimali hizo za ziada zitagharamia hatua mahususi za kukabiliana na Ebola, ikiwa ni pamoja na mafunzo ya kivitendo ya kuzuia na kudhibiti maambukizi (IPC) kwa wahudumu wa afya walio mstari wa mbele, ununuzi na usambazaji wa vifaa maalum vya kujikinga (PPE) dhidi ya Ebola, kuimarisha utayari wa kikanuni ili kuharakisha upatikanaji wa chanjo zinazoweza kutumika dhidi ya Ebola, dawa na hatua nyingine za kimatibabu, pamoja na shughuli za kuielimisha jamii ili kupunguza kusita kupokea chanjo na kuunga mkono kampeni zijazo za chanjo dhidi ya Ebola.

Alibainisha kuwa hatua zote zitatekelezwa kwa ushirikiano wa karibu na Sekretarieti ya EAC pamoja na nchi husika wanachama, na zitaendana na Mpango wa Bara wa Kujiandaa na Kukabiliana na Ebola unaoongozwa na Africa CDC na WHO, ili kuhakikisha kunakuwa na ufanisi unaokamilisha juhudi za kikanda na kimataifa za kukabiliana na janga hilo.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3