Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
FADHILI TEENS YAZINDUA MRADI WA MOTISHA KWA WALIMU MKOANI MWANZA

FADHILI TEENS YAZINDUA MRADI WA MOTISHA KWA WALIMU MKOANI MWANZA

 


NA CHAUSIKU SAID 

MATUKIO DAIMA MWANZA.

Taasisi isiyo ya kiserikali ya Fadhili Teens Tanzania imezindua mradi maalumu wa kutoa motisha kwa walimu wa shule za sekondari katika Halmashauri za Magu na Buchosa mkoani Mwanza, ukiwa na lengo la kuongeza hamasaa ya ufundishaji na kuboresha ufaulu wa wanafunzi.

Uzinduzi wa mradi huo umefanyika Agosti 4, 2026 katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu ukihusisha wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo maafisa elimu, wakuu wa shule na wakuu wa idara kutoka shule mbalimbali ikiwa umezinduliwa rasmi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mohamed Ramadhan. 


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mkurugenzi kutoka Wilaya ya Magu Mohamed Ramadhan amewataka wadau wa elimu kushirikiana kwa karibu na wazazi ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya katika sekta ya elimu. 

Amesema kuwa mafanikio ya mwanafunzi yanategemea kwa asilimia 75 juhudi zake binafsi huku asilimia 25 zikichangiwa na mazingira yanayomzunguka, ikiwemo uwepo wa walimu wenye motisha, miundombinu bora na mazingira mazuri ya kujifunzia pia amesisitiza kuwa ni muhimu kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira rafiki yatakayowawezesha kufanya vizuri katika masomo yao. 

Salome Ndimila kutoka Fadhili Teens Tanzania

Awali akieleza malengo ya mradi huo, Salome Ndimila kutoka Fadhili Teens Tanzania amesema mradi utatekelezwa katika shule 20, ambapo shule 10 zinatoka Halmashauri ya Buchosa na shule 10 kutoka Halmashauri ya Magu. 

Amefafanua kuwa mradi huo unatarajiwa kuwafikia walimu 300, wanafunzi 10,000 pamoja na wazazi 8,000. 


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mohamed Ramadhan

Aidha, taasisi hiyo itatoa mafunzo ya kuwajengea uwezo walimu na jamii kwa kushirikiana na Serikali kwa lengo la kuboresha mbinu za ufundishaji na kuongeza ufaulu wa wanafunzi. 


Baadhi ya washiriki wa mradi huo, akiwemo Mwalimu Kaombwe Edward na Mwalimu Christina Nisa wameishukuru Fadhili Teens Tanzania kwa kuanzisha mradi huo na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha unatekelezwa kwa mafanikio na kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3