BONANZA LA BUNGE KULENGA AFYA NA MSHIKAMANO WA WATUMISHI
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
WIZARA 14 na Taasisi 10 zinatarajiwa kushiriki katika Bonanza la Michezo la Bunge la 13 litakalofanyika kesho jijini Dodoma, likilenga kuimarisha afya, mshikamano na mahusiano ya kikazi miongoni mwa wabunge, watumishi wa Bunge na taasisi mbalimbali za Serikali.
Bonanza hilo litafanyika kuanzia saa 12:00 asubuhi katika Viwanja vya Mipango, eneo la John Merlin Secondary School, ambapo washiriki watashindana katika michezo mbalimbali ikiwamo mpira wa wavu, mpira wa pete, kikapu, kuvuta kamba na mbio, sambamba na burudani.
Akizungumza na waandishi wa habari Bungeni Dodoma kuhusu maandalizi ya bonanza hilo, Mbunge wa Jimbo la Makete na Mwenyekiti wa Bonanza la Michezo la Bunge, Festo Richard Sanga, amesema maandalizi yamekamilika na washiriki kutoka taasisi mbalimbali wamejiandaa kwa ajili ya mashindano hayo.
Sanga amesema bonanza hilo limeandaliwa ikiwa ni sehemu ya juhudi za Bunge kuendeleza michezo miongoni mwa watumishi wake na wakati huo huo kutoa fursa ya kujenga mahusiano na taasisi zinazoshirikiana nalo.
Amesema mgeni rasmi katika bonanza hilo anatarajiwa kuwa Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azzan Zungu, ambaye atakuwa sehemu ya tukio hilo linalolenga kuunganisha watumishi na wadau mbalimbali kupitia michezo.
Amesema michezo ni nyenzo muhimu katika kuimarisha afya ya mwili na akili, huku ikitoa nafasi kwa watumishi kukutana katika mazingira yasiyo rasmi na kujenga urafiki na mshikamano.
Kwa upande wa udhamini, Benki ya NMB imewekeza Sh210 milioni katika kufanikisha bonanza hilo, ikiwa ni sehemu ya ushirikiano wake na Bunge pamoja na dhamira yake ya kushiriki katika shughuli zinazolenga kuleta thamani kwa jamii.
Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano ya Benki na Serikali wa NMB, Vicky Bishubo, amesema ushirikiano kati ya benki hiyo na Bunge una historia ndefu na umejengwa katika misingi ya mahusiano ya kimkakati.
Bishubo amesema NMB inatambua nafasi ya Bunge katika maendeleo ya Taifa na itaendelea kushirikiana nalo katika shughuli mbalimbali zenye manufaa kwa jamii.
“Mahusiano yetu na Bunge ni ya kihistoria na kama mashirika ya kimkakati tunayathamini. Tunaahidi kuendelea kuboresha huduma zetu kwa jamii na wakati wowote tunahitaji muendelee kutushirikisha,” amesema Bishubo.
Amesema Sh210 milioni zilizowekezwa katika bonanza hilo ni sehemu ya dhamira ya NMB ya kurudisha thamani kwa jamii, huku michezo ikiwa miongoni mwa maeneo yanayoweza kuunganisha watu, kuhamasisha maisha yenye afya na kujenga mahusiano.
Bishubo amesema NMB imewezesha mahitaji mbalimbali ya bonanza hilo, ikiwamo vifaa vya michezo, mipira na vikombe vya washindi, ili kuhakikisha mashindano yanafanyika katika mazingira bora.
Amesema jukumu la NMB katika jamii haliishii katika kutoa huduma za kifedha pekee, bali benki hiyo pia inashiriki katika shughuli za kijamii zinazolenga kuboresha ustawi wa wananchi.
Kwa upande wake, Sanga amesema ushiriki wa wizara na taasisi hizo unalifanya bonanza hilo kuwa jukwaa la kuimarisha mahusiano ya kitaasisi, huku washiriki wakipata nafasi ya kubadilishana uzoefu na kujenga mshikamano.
Amesema pamoja na ushindani, bonanza hilo litakuwa na burudani mbalimbali zitakazowapa washiriki na wageni nafasi ya kufurahia tukio hilo.
Bonanza hilo linatarajiwa kuwa zaidi ya mashindano ya michezo, kwani litatoa fursa ya kuhamasisha maisha yenye afya na kuimarisha mahusiano kati ya Bunge, Serikali na sekta binafsi.



