BODI YA PAMBA KUTUMIA MAONESHO YA NANENANE KUHAMASISHA TEKNOLOJIA YA KISASA NA KUONGEZA THAMANI YA DHAHABU NYEUPE.
NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nyamhongoro, Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza, yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwajengea uwezo wakulima na wadau wa zao la pamba kupitia elimu ya teknolojia za kisasa na mnyororo wa thamani wa zao hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa Kilimo kutoka Bodi ya Pamba Tanzania, Dotto Ntumba, amesema maonesho hayo yanalenga kuwafikia wakulima na wadau mbalimbali wa zao la pamba kwa kuwapa elimu itakayowasaidia kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa pamba na kuongeza kipato.
Ntumba amesema Bodi ya Pamba imeandaa shamba darasa litakalowawezesha wakulima kujifunza mbinu bora za kilimo cha pamba kuanzia maandalizi ya shamba, matumizi sahihi ya mbegu bora, udhibiti wa magonjwa na wadudu waharibifu hadi matumizi ya teknolojia mpya zinazorahisisha uzalishaji.
Ameeleza kuwa miongoni mwa teknolojia hizo ni matumizi ya vifaa vya kisasa vya kunyunyizia viuatilifu pamoja na ndege zisizo na rubani (drones), ambazo husaidia kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza ufanisi wa upuliziaji wa dawa na kulinda afya ya mkulima.
Kwa mujibu wa Ntumba, ameeleza kuwa elimu inayotolewa haijajikita katika uzalishaji pekee, bali pia inaelekeza wadau kutambua fursa zilizopo katika mnyororo mzima wa thamani wa zao la pamba, kuanzia shambani hadi viwandani.
Ameeleza kuwa baada ya pamba kuvunwa hupelekwa katika viwanda vya kuchambua ambapo hupatikana bidhaa kuu mbili ambazo ni nyuzi za pamba na mbegu ambapo nyuzi hutumika katika uzalishaji wa nguo na bidhaa nyingine za viwandani, huku mbegu zikitumika kwa ajili ya kupanda msimu unaofuata.
Aidha amefafanua kuwa uzalishaji wa miaka ya nyuma zaidi ya asilimia 80 ya pamba iliyozalishwa nchini ilisafirishwa nje kama malighafi, kwa sasa matumizi ya ndani yameongezeka na zaidi ya asilimia 30 ya uzalishaji hutumika na viwanda vya ndani kutokana na juhudi za Serikali kufufua na kujenga viwanda vya nguo. Kwa mujibu wa Bodi ya Pamba Tanzania, kuongezeka kwa viwanda vya kuchakata pamba nchini kutasaidia kuongeza thamani ya zao hilo.


