WANAFUNZI WA ST. DOMINIC SAVIO WATEMBELEA MAMA NGINA WATERFRONT GARDEN NCHINI KENYA
NA MATUKIO DAIMA MEDIA ,KENYA
ZAIDI ya wanafunzi 80 kutoka Shule za St. Dominic Savio zilizopo Iringa, Tanzania, wameendelea na ziara yao ya kimasomo nchini Kenya kwa kutembelea eneo maarufu la Mama Ngina Waterfront Garden lililopo jijini Mombasa. Ziara hiyo imelenga kuwapa wanafunzi nafasi ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii pamoja na maendeleo ya miundombinu ya nchi jirani.
Wakiwa katika bustani hiyo maarufu, wanafunzi walipata fursa ya kushiriki michezo mbalimbali ya kisasa na burudani za viwango vya juu. Baadhi yao walifurahia kupanda ngamia, magari ya watoto na treni za umeme, huku wengine wakijionea mandhari ya kuvutia ya Bahari ya Hindi.
Eneo hilo limekuwa kitovu cha burudani kwa watoto, vijana na watu wazima, likiwavutia maelfu ya watalii na wakazi wa Mombasa kila mwaka.
Mama Ngina Waterfront Garden limepewa jina la Mama Ngina Kenyatta, mjane wa Rais wa kwanza wa Kenya, Hayati Jomo Kenyatta, ambaye bado ni mmoja wa viongozi wa heshima katika historia ya taifa hilo. Bustani hiyo ni sehemu muhimu ya mapumziko na burudani kwa wananchi na wageni wanaotembelea Mombasa.
Aidha, eneo hilo linapatikana karibu na kivuko cha Likoni, ambapo wasafiri wanaovuka bahari kwa kutumia ferry hupata nafasi ya kupumzika na kufurahia mazingira mazuri kabla au baada ya safari zao.
Wageni pia hupata huduma mbalimbali zikiwemo vyakula vya baharini, vinywaji na bidhaa nyingine zinazouzwa na wafanyabiashara wa eneo hilo.
TAZAMA VIDEO BOFYA LINK HIIKwa wanafunzi wa St. Dominic Savio, ziara hiyo imekuwa sehemu ya mafunzo yanayowawezesha kujifunza historia, jiografia, utamaduni na sekta ya utalii wa Kenya kwa njia ya vitendo.
Walionyesha furaha kubwa kwa kupata uzoefu mpya na kushiriki shughuli mbalimbali zilizowaongezea maarifa na kuwajengea kumbukumbu nzuri.
Shule za St. Dominic Savio za Iringa zimeendelea kujijengea sifa nchini Tanzania kutokana na kutoa elimu bora inayozingatia ubora wa kitaaluma pamoja na kuwapa wanafunzi nafasi ya kujifunza nje ya darasa kupitia ziara za kielimu ndani na nje ya nchi.
Ziara hiyo nchini Kenya ni uthibitisho wa dhamira ya shule hiyo ya kuandaa wanafunzi wenye maarifa mapana, ujasiri na uwezo wa kushindana katika mazingira ya kimataifa.





