Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WADAU WAPENDEKEZA MABORESHO  BIASHARA MTANDAONI KUKUZA UCHUMI WA KIDIGITAL

WADAU WAPENDEKEZA MABORESHO BIASHARA MTANDAONI KUKUZA UCHUMI WA KIDIGITAL

 

Na Matukio Daima Media 

Wadau wa biashara mtandaoni wameiomba Serikali kuharakisha maboresho ya sera, sheria na mifumo ya kidijitali ili kuondoa vikwazo vinavyokwamisha biashara za mtandaoni na kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.

Mapendekezo hayo yametolewa leo Julai 31,2026 katika Mkutano wa siku mbili uliowakutanisha wawakilishi wa Serikali, sekta binafsi, taasisi za utafiti, vyuo vikuu na wataalamu wa teknolojia kujadili namna ya kuimarisha mazingira ya biashara mtandaoni nchini.


Akizungumza na waandishi wa habari kando ya mkutano huo Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Dk. Nkundwe  Mwasaga, amesema biashara mtandaoni ni moja ya sekta zinazokua kwa kasi na zina uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira kwa vijana pamoja na kuongeza ushindani wa uchumi wa Tanzania.


Amesema Tanzania ina zaidi ya kampuni ndogo na za kati milioni tatu, huku soko la biashara mtandaoni likiwa na thamani ya takribani dola za Marekani milioni 600 mwaka uliopita na linatarajiwa kuendelea kukua kwa wastani wa asilimia 10 hadi 15.


"Dira ya Taifa inaonyesha wazi kuwa mapinduzi ya kidijitali ni nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi. Biashara mtandaoni ni sehemu muhimu ya mapinduzi hayo na inatoa fursa kubwa kwa vijana na wafanyabiashara," amesema.


Dk. Mwasaga amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali, ikiwemo mifumo ya utambulisho wa kidijitali na Tanzania Instant Payment System (TIPS), huku akiwataka vijana kutumia fursa hizo kuanzisha biashara na ubunifu wa kidijitali.



Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara(TNBC)Dk. Godwill  Wanga, amesema pamoja na fursa zilizopo, bado kuna changamoto zinazohitaji kutatuliwa, ikiwemo mifumo ya ulipaji kodi, ucheleweshaji wa usafirishaji wa bidhaa na gharama za miamala ya kifedha.


Amesema wadau wamependekeza majukwaa ya kimataifa ya biashara mtandaoni yaunganishwe na mifumo ya mamlaka za kodi ili kurahisisha ukusanyaji wa mapato, huku kampuni kubwa zikihimizwa kuanzisha maghala ya bidhaa nchini ili kupunguza muda wa kuwafikishia wateja bidhaa walizoagiza.


"Katika biashara za kidijitali, mteja anatarajia kupata bidhaa kwa haraka. Ni muhimu kuboresha mifumo ya usafirishaji na malipo ili kuongeza ufanisi wa biashara mtandaoni," amesema  Dr.Wanga


Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Haki Bunifu Afrika (Africa Research Institute for AI (ARIFA) Eng.Dr.Dennis Mwighusa amesema pamoja na maendeleo ya Teknolojia, Tanzania bado inahitaji kuwa na sera maalumu ya biashara mtandaoni pamoja na mifumo madhubuti ya sheria na miongozo itakayowezesha sekta hiyo kukua kwa kasi.


"Tunahitaji sera ya taifa ya biashara mtandaoni pamoja na mifumo imara ya sheria na miongozo itakayosaidia kukuza biashara za kidijitali na kulinda maslahi ya wadau wote," amesema.


Mwighusa amesema mafanikio ya uchumi wa kidijitali hayatategemea uwepo wa sera pekee, bali pia utekelezaji wake, huku akisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika elimu ya matumizi ya teknolojia na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za elimu na wataalamu wa teknolojia.


Wadau hao wameeleza kuwa utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa utasaidia kupunguza gharama za kufanya biashara, kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa na kuifanya biashara mtandaoni kuwa nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3