VITUMBUA FESTIVAL YAZINDULIWA, WASHINDI KUNUFAIKA NA KIWANJA NA FEDHA TASLIMU
Umoja wa Mama na Baba Lishe Tanzania (UMALITA) umetangaza kuanzisha tamasha jipya la Vitumbua Festival, litakalofanyika Julai 30, 2026 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, likiwa na lengo la kuinua hadhi ya wachoma vitumbua, kuongeza thamani ya biashara hiyo na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa UMALITA Taifa, Avijawa Omary alisema tamasha hilo litawakutanisha wachoma vitumbua kutoka wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam katika mashindano yatakayolenga kutambua ubunifu na kuwapa motisha wajasiriamali hao.
Alisema mshindi wa kwanza atajishindia fedha taslimu, kiwanja pamoja na eneo maalumu la kufanyia biashara ya vitumbua, huku washindi wa pili na wa tatu wakipatiwa fedha taslimu, vifaa vya biashara na zawadi nyingine mbalimbali.
"Tunataka kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu biashara ya vitumbua kwa kutambua mchango wake katika kukuza uchumi wa familia, kuajiri vijana na wanawake pamoja na kuchochea maendeleo ya sekta ya ujasiriamali," alisema Avijawa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa UMALITA, Johajulieth Madata, alisema tamasha hilo pia litatumika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, ambapo washiriki wote watapatiwa elimu kuhusu matumizi ya gesi ya kupikia (LPG).
Alieleza kuwa matumizi ya gesi badala ya kuni na mkaa yatasaidia kulinda mazingira, kuboresha afya za wachoma vitumbua, kuongeza usafi katika maandalizi ya chakula na kuinua tija ya biashara zao.Aidha, baadhi ya wajasiriamali wanaojishughulisha na biashara ya vitumbua wameeleza matumaini yao kuwa tamasha hilo litakuwa chachu ya kutangaza bidhaa zao, kuwafungulia masoko mapya na kuboresha mazingira ya kazi pamoja na kipato chao.

.jpeg)
.jpeg)