Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
UMALITA YATUMIA VITUMBUA FESTIVAL KUHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI

UMALITA YATUMIA VITUMBUA FESTIVAL KUHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI

 
Na Matukio DaimaMedia 

Umoja wa Mama na Baba Lishe Tanzania (UMALITA) umesema Tamasha la Vitumbua Festival limekuwa chachu ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuwawezesha mama na baba lishe kuboresha biashara zao.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika na tamasha hilo, Mwenyekiti wa UMALITA, Avijawa Omary,  amesema washindi walikabidhiwa fedha taslimu na zawadi mbalimbali kama ilivyoahidiwa, huku akiwashukuru wadhamini wakiwemo SCCF, NMB Bank, Benki ya Azania, Simba Gas na TIA kwa kufanikisha tamasha hilo.

Amesema umoja huo utaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha mama na baba lishe wanapata elimu, mitaji na fursa zitakazowawezesha kukuza biashara zao na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.


Aidha, amesema umoja huo umekamilisha maandalizi ya mfumo wa kidijitali wa UMALITA App, utakaosaidia kuwaunganisha wanachama na huduma mbalimbali za biashara.

Kwa upande wake, Katibu wa UMALITA, Johajulieth Madata, amesema tamasha hilo lilitanguliwa na kampeni ya mwezi mmoja ya kutoa elimu kwa mama na baba lishe katika masoko na mitaa mbalimbali kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Madata amesema baada ya tamasha hilo, UMALITA itaendelea kuwawezesha mama na baba lishe kwa kuwaunganisha na huduma za bima ya afya, mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja na mikopo yenye masharti nafuu ili kuboresha maisha yao

Amesema pamoja na kutoa elimu, umoja huo ulitoa mitungi ya gesi kwa baadhi ya wafanyabiashara ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi, huku lengo kuu likiwa ni kulinda afya za wafanyabiashara hao na mazingira.


"Tulipita soko kwa soko na mtaa kwa mtaa kutoa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi, Lengo halikuwa kugawa mitungi pekee, bali kuhakikisha mama na baba lishe wanaelewa umuhimu wa kutumia nishati safi katika shughuli zao za kila siku," amesema.

Amesema juhudi hizo ziliifanya UMALITA kutunukiwa tuzo na Ofisi ya Makamu wa Rais kutokana na mchango wake katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini.

Madata amesema tamasha hilo pia lililenga kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu biashara ya vitumbua kwa kuonyesha kuwa inaweza kufanywa kwa kuzingatia ubora, usafi na kuwa chanzo cha kipato.

Katika mashindano hayo, mshiriki kutoka Wilaya ya Kigamboni aliibuka mshindi baada ya kuonyesha umahiri katika upishi wa vitumbua na kukidhi vigezo vilivyowekwa na waandaaji.


Mmoja wa majaji wa mashindano hayo, Afua Juma, maarufu kama Mama Nyema, amesema ushindani ulikuwa mkubwa kutokana na washiriki wengi kuonyesha kiwango kizuri cha umahiri katika upishi wa vitumbua.

"Nimekuwa nikipika vitumbua kwa zaidi ya miaka 10. Washiriki wote wamejitahidi na waliopata ushindi walistahili kutokana na ubora waliouonyesha," amesema.


Amesema tamasha hilo limewapa motisha wachoma vitumbua kuendelea kuboresha biashara zao baada ya washiriki wengi kuondoka na fedha taslimu pamoja na zawadi mbalimbali.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3